Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imejizatiti kwenye
uwekezaji mkubwa wa miradi ya maendeleo ukiwemo wa Shilingi trilioni mbili katika Ujenzi wa miundombinu ya umeme mkoani Mbeya, akisema hatua hiyo ni sehemu ya dhamira ya Serikali ya kuleta mapinduzi ya kiuchumi kupitia upatikanaji wa nishati ya uhakika.
Makamu wa Rais ameyasema hayo leo, Oktoba 16, 2026, wakati alipotembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa Kituo cha Kupokea na Kusambaza Umeme cha Iganjo mkoani Mbeya, ambacho ni miongoni mwa miradi ya kimkakati inayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita kwa lengo la kuimarisha upatikanaji wa umeme na kuchochea shughuli za kiuchumi nchini.
Amesema uwekezaji huo mkubwa unaofanywa na Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. hautawanufaisha wananchi wa Mbeya pekee, bali pia utafungua fursa za uwekezaji katika sekta ya madini, viwanda na biashara, huku ukiwezesha Tanzania kusambaza umeme katika nchi jirani na kulifanya Jiji la Mbeya kuwa kitovu muhimu cha kiuchumi katika Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).
Ameeleza kuwa kukamilika kwa miradi hiyo kutalipa Jiji la Mbeya hadhi halisi ya kuwa lango la SADC, kutokana na nafasi yake ya kimkakati katika kuunganisha shughuli za kiuchumi na biashara kati ya Tanzania na mataifa mengine ya ukanda wa Kusini mwa Afrika.
Aidha, Makamu wa Rais ameipongeza Wizara ya Nishati pamoja na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa usimamizi na utekelezaji wa mradi huo, akieleza kuridhishwa na kasi ya ujenzi na kuonesha matumaini kuwa ifikapo Desemba 2026, kituo hicho kitakuwa kimewashiwa umeme na kuanza kuleta manufaa kwa wananchi.
Amesisitiza kuwa Serikali inaendelea kutekeleza kwa vitendo ahadi zake kwa wananchi kupitia miradi mikubwa ya maendeleo, huku akiwahimiza watendaji na wafanyakazi wanaotekeleza mradi huo kuongeza juhudi, kufanya kazi kwa bidii na kuhakikisha unakamilika kwa wakati ili wananchi waanze kunufaika na uwekezaji huo.
Akiwasilisha Taarifa ya maendeleo ya Mradi, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Lazaro Twange, amesema ujenzi wa Kituo cha Iganjo unaogharimu Shilingi bilioni 175.7, hadi kufikia Oktoba 11, 2026 mradi umefikia asilimia 89.25 ya utekelezaji huku kampuni ya TBEA kutoka China inayotekeleza mradi huo ikitarajiwa kukamilisha kazi za kuwasha umeme kituoni hapo mwezi Novemba 2026.
Twange ameeleza kuwa kituo hicho kitakuwa na uwezo wa kupokea na kupunguza msongo wa umeme kutoka kilovolti 400 hadi 220 na 33, hatua itakayosaidia kuimarisha upatikanaji wa umeme katika mikoa ya Mbeya na Songwe, kuchochea uzalishaji viwandani na kuhudumia shughuli za uchimbaji madini katika maeneo ya Saza na Chunya.
Ameongeza kuwa kituo hicho kitakuwa na umuhimu mkubwa katika kuunganisha vyanzo vipya vya uzalishaji umeme vya Rumakali, Ngozi na Kiwila kwenye Gridi ya Taifa, pamoja na kuwezesha uunganishaji wa gridi za umeme za Tanzania na Malawi kwa ajili ya biashara ya umeme, hatua itakayoongeza nafasi ya Tanzania katika soko la nishati la kikanda.
Naye Mbunge wa Jimbo la Uyole ambaye pia ni Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Tulia Ackson, ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji huo mkubwa, akisema mradi wa Iganjo ni fahari kwa wananchi wa Uyole, Mkoa wa Mbeya na Taifa kwa ujumla.
Dkt. Tulia amesema utekelezaji wa mradi huo ni kielelezo cha dhamira ya Serikali ya kupeleka maendeleo kwa wananchi kupitia uwekezaji katika miundombinu muhimu, hususan nishati ya umeme ambayo ni kichocheo kikubwa cha ukuaji wa uchumi na ustawi wa jamii.
Ziara ya Makamu wa Rais mkoani Mbeya ni sehemu ya juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita za kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo, kuhakikisha fedha zinazowekezwa zinaleta matokeo yaliyokusudiwa, pamoja na kusikiliza na kutatua kero mbalimbali zinazowakabili wananchi.
