Na Mwamvua Mwinyi, Bagamoyo
WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba, amemuagiza Kamishna wa Ardhi Tanzania Nathaniel Mathew Nhonge kufika Bagamoyo Oktoba 19, 2026, kuongoza kliniki maalumu ya kusikiliza na kutatua kero za ardhi zinazowakabili wananchi wa wilaya hiyo.
Ametaka Kamishna huyo kufika mwenyewe akiwa na timu kutoka makao makuu, kwa kushirikiana na wataalamu wa mkoa, Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), ili kushughulikia malalamiko ya wananchi kwa wiki nzima.
“Usitume mwakilishi, uje mwenyewe kusikiliza mtu mmoja mmoja wewe mwenyewe,” amesema Mwigulu.
Amesema migogoro ya ardhi inatishia undugu na mshikamano katika jamii, hivyo amewaelekeza Waziri wa Ardhi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Waziri anayesimamia TAMISEMI kupitia upya utaratibu wa kushughulikia migogoro hiyo ili kupata suluhisho la kudumu.
Kuhusu wananchi wanaopisha maeneo kwa ajili ya uwekezaji na miradi ya maendeleo, Waziri Mkuu amesisitiza umuhimu wa kulipwa fidia stahiki bila kupunjwa, akieleza kuwa haki zao zinapaswa kulindwa wakati wa utekelezaji wa miradi hiyo.
Aidha, ameliagiza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuendelea kuwaunganishia umeme kwa gharama ya Sh. 27,000 wananchi wanaoishi katika maeneo yaliyopandishwa hadhi kuwa miji midogo, lakini bado wanaishi katika mazingira yanayofanana na vijijini.
Amesema mabadiliko ya hadhi ya maeneo hayo hayamaanishi kuwa wananchi wameongezewa uwezo wa kiuchumi, hivyo hawapaswi kunyimwa fursa ya kupata huduma ya umeme kwa gharama wanayoweza kumudu.
“Wananchi hawa wanaoitwa mji mdogo niwaelekeze watu wa TANESCO, umeme waendelee kuunganishiwa kwa 27,000 ile ile ya kijijini,” amesisitiza.
Kuhusu urasimishaji wa Bagamoyo, Dkt. Mwigulu amewahakikishia wananchi kuwa hati ya kuirasimisha inatarajiwa kupatikana wiki ijayo, akisema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan tayari amefanya uamuzi na kinachosubiriwa ni kukamilika kwa taratibu zilizobaki.
Ametoa maagizo hayo Oktoba 16, 2026, alipozungumza na wananchi mjini Bagamoyo, mkoani Pwani, wakati wa ziara yake ya kikazi ya siku moja.

