Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, ameiagiza Wizara ya Kilimo kuchukua hatua za haraka kuchunguza sababu za kushuka kwa bei ya mahindi na kutafuta ufumbuzi wa changamoto hiyo, kufuatia malalamiko ya wakulima kuhusu bei ndogo ya zao hilo.
Makamu wa Rais ametoa maelekezo hayo wakati akizungumza na wananchi wa Jimbo la Vwawa na Mlowo mkoani Songwe, Wilaya ya Mbozi, wakati wa ziara yake ya kikazi inayolenga kusikiliza kero za wananchi na kufuatilia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
Amesema Wizara ya Kilimo inapaswa kulifanyia kazi suala hilo kwa haraka, ikiwemo kubaini sababu zinazochangia bei ndogo ya mazao, ili kuwezesha kupatikana kwa ufumbuzi utakaosaidia kukabiliana na changamoto zinazowakabili wakulima.
Katika hatua nyingine, Makamu wa Rais amewataka viongozi na watendaji wa Serikali kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo, hususan katika sekta za umeme, maji na miundombinu ya barabara, ambazo zimeendelea kutajwa na wananchi kuwa miongoni mwa changamoto kubwa zinazohitaji ufumbuzi.
Amesisitiza umuhimu wa watendaji wa Serikali kutekeleza kwa vitendo mipango na vipaumbele vya Serikali ya Awamu ya Sita, inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuhakikisha huduma muhimu za kijamii na kiuchumi zinawafikia wananchi kwa wakati.
Makamu wa Rais amesema juhudi za Serikali katika kuboresha maisha ya wananchi zinapaswa kuendana na uwajibikaji wa viongozi na watendaji katika kushughulikia changamoto zinazojitokeza kwenye maeneo yao ya kazi.
Katika ziara hiyo, Makamu wa Rais ameambatana na mawaziri wanaosimamia sekta mbalimbali, wakiwemo wa Nishati, Maji, Ujenzi na Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).
Kupitia mikutano ya hadhara iliyofanyika katika maeneo hayo, mawaziri hao wamepata fursa ya kusikiliza na kujibu hoja zilizowasilishwa na wananchi, huku wakieleza hatua zinazochukuliwa na Serikali kushughulikia changamoto zinazohusu sekta zao.
Wakati huohuo, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Patrobas Katambi, ameeleza hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Wizara yake akiwataka wananchi kuendelea kulinda amani, umoja na utulivu wa nchi kwa kujiepusha na vitendo vinavyoweza kuhatarisha usalama wa jamii.
Amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kusimamia sheria na kuchukua hatua stahiki dhidi ya watu watakaobainika kujihusisha na vitendo vya uvunjifu wa amani.
Aidha, amewahimiza wananchi kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama katika kudumisha utulivu, akisisitiza umuhimu wa kila mwananchi kutimiza wajibu wake katika kulinda amani na mshikamano wa taifa.
Makamu wa Rais anaendelea na ziara ya kikazi katika Mikoa ya Songwe na Mbeya akitokea mkoani Rukwa kumwakilisha Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwenye kilele cha mbio za Mwenge wa Uhuru 2026 sambamba na kumbukizi ya miaka 27 ya kifo cha Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

