Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, akikabidhiwa jezi ya Real Madrid na Mkurugenzi Mtendaji wa Real Madrid Foundation, Bw. Julio González Ronco, wakati wa hafla ya utiaji saini wa makubaliano baina ya Real Madrid Foundation na Unicorn Zanzibar Sports Limited, iliyofanyika tarehe 13 Oktoba 2026, jijini Madrid, Uhispania.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, akikabidhiwa jezi ya Real Madrid na nguli wa soka wa Brazil na mchezaji wa zamani wa klabu hiyo, Roberto Carlos, katika viwanja vya mazoezi vya Real Madrid, wakati wa hafla ya utiaji saini wa makubaliano baina ya Real Madrid Foundation na Unicorn Zanzibar Sports Limited, iliyofanyika tarehe 13 Oktoba 2026, jijini Madrid, Uhispania.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, akikabidhiwa jezi ya Real Madrid na Rais wa klabu hiyo, Bw. Florentino Pérez, katika Uwanja wa Santiago Bernabéu, jijini Madrid, Uhispania, tarehe 10 Oktoba 2026, alipohudhuria mchezo kati ya Real Madrid na Villarreal CF.

Rais Dkt. Mwinyi ameshuhudia utiaji saini wa makubaliano baina ya Real Madrid Foundation na Unicorn Zanzibar Sports Limited kuhusu kuendeleza vipaji vya soka kwa vijana Zanzibar.

…………

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema ushirikiano kati ya Real Madrid Foundation na Unicorn Zanzibar Sports Limited utafungua fursa za vijana wa Kizanzibari kukuza vipaji vya soka kupitia mafunzo yanayounganisha michezo, nidhamu na maadili.

Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, tarehe 13 Oktoba 2026, mjini Madrid, nchini Uhispania, katika hafla utiaji saini wa Hati ya Makubaliano baina ya taasisi hizo, inayolenga kuanzisha programu maalumu za mafunzo ya soka kwa vijana Zanzibar.

Amesema Serikali imeendeleza zaidi ya viwanja 30 vya mpira wa miguu katika maeneo mbalimbali ya Zanzibar, na hatua inayofuata ni kuunganisha uwekezaji huo na maarifa, mbinu za ufundishaji na uzoefu wa kimataifa ili kuwasaidia vijana kufikia uwezo wao.

Rais Dkt. Mwinyi amesisitiza kuwa kipaji pekee hakitoshi kumfikisha kijana kwenye mafanikio bila mwalimu bora, nidhamu, elimu, miundombinu na mfumo unaotambua na kuendeleza uwezo wake. Ameeleza kuwa dhamira ya Serikali ni kuhakikisha vijana wanapata mazingira yanayowawezesha kukuza vipaji na kutimiza ndoto zao.

Aidha, Rais Dkt. Mwinyi amesema mafanikio ya programu hizo hayatapimwa kwa idadi ya vijana watakaokuwa wachezaji wa kulipwa pekee, bali pia kwa mchango wake katika kuwajengea nidhamu, kujiamini, kuheshimu wengine na kuwa na dhamira ya kutimiza malengo yao.

Amesema Serikali itaendelea kuwekeza katika miundombinu ya michezo, kuendeleza vijana na kuimarisha ushirikiano unaoleta maarifa, uzoefu na fursa mpya Zanzibar, huku akieleza kuwa ana matumaini ya kuona vijana wa Zanzibar wakifikia viwango vya juu vya soka duniani.

Naye, Mwenyekiti wa Unicorn Sports, Bw. Sergio Garcia, amesema kampuni hiyo inalenga kuanza na mafunzo maalumu ya soka, yakifuatiwa na kuanzishwa kwa akademia ya kudumu katika Viwanja vya Michezo Zanzibar. Ameeleza kuwa mpango huo unakusudia kuwaleta makocha wenye uzoefu kutoka Real Madrid kufanya kazi pamoja na makocha wa ndani watakaopatiwa mafunzo kupitia programu hiyo, huku akiishukuru Serikali kwa kuwezesha matumizi ya miundombinu hiyo katika utekelezaji wa mradi.

Naye, Makamu Mwenyekiti wa Unicorn Sports, Bw. Mohamed Sleiman, amesema matarajio yao ni kupanua wigo wa programu hiyo ili kuwafikia vijana wa kike na wa kiume kutoka maeneo mbalimbali ya Zanzibar, hususan wenye vipaji ambao bado hawajapata fursa za kuviendeleza. 

Rais Dkt. Mwinyi amekamilisha ziara yake ya kikazi nchini Uhispania, ikiwa ni mwendelezo wa ziara iliyoanzia Doha, Qatar. Leo, tarehe 13 Oktoba 2026, anaondoka kuelekea nchini Armenia, ambako anatarajiwa kushiriki Mkutano wa Viongozi wa PIN (PIN Leaders Summit).