NA SOPHIA KINGIMALI, DAR ES SALAAM

SERIKALI ya Tanzania imetangaza kuwa itakuwa mwenyeji wa ujenzi Chuo Kikuu cha Kikanda cha Usafiri kwa Njia ya Maji (Regional Maritime University – RMU), hatua inayolenga kuimarisha elimu, mafunzo, utafiti na ubunifu katika sekta ya usafiri wa majini barani Afrika.

Akitoa taarifa hiyo kwa niaba ya Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile, amesema Tanzania ipo tayari kushirikiana na nchi wanachama wa Shirika la Usafiri wa Majini la Afrika Mashariki, Kusini na Kaskazini (MOWCA) kuhakikisha chuo hicho kinakuwa kituo cha umahiri wa kikanda.

Kihenzile alitoa taarifa hiyo jijini Dar es Salaam, leo Oktoba 13, 2026, kuelekea mkutano wa 10 wa kawaida wa Baraza la Mawaziri la Shirikala masuala ya ya usafiri wa majini kwa Afrika mashariki, Kusini na Kasazini(MOESNA), unaotarajiwa kufanyika Oktoba 15 mwaka huu, ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu Dkt Mwigulu Nchema na kuhudhuriwa na takribani mawaziri 26 wanaosimamia sekta za uchukuzi na usafirishaji wa mizigo.

Amesema mkutano huo utajadili masuala mbalimbali ya kuimarisha biashara baina ya nchi wanachama, hususan kupitia usafirishaji wa mizigo na abiria kwa njia ya maji, pamoja na kuimarisha uhusiano wa kibiashara kati ya nchi zisizo na mwambao wa bahari na zile zenye bandari.

Alieleza kuwa mkutano huo utahusisha nchi wanachama pamoja na wawakilishi wa taasisi za kikanda na kimataifa, zikiwemo Umoja wa Afrika (AU), Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), sekretarieti ya Eneo Huru la Biashara Barani Afrika (AfCFTA), Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

Aidha Kihenzile amesema, usafiri wa majini ni nguzo muhimu katika kukuza biashara ya kimataifa, ikizingatiwa kuwa zaidi ya asilimia 90 ya biashara ya nje ya Afrika husafirishwa kwa njia ya bahari, huku zaidi ya asilimia 80 ya biashara ya bidhaa duniani kwa ujazo ikitegemea usafiri huo.

Amesema maendeleo ya biashara barani Afrika yanahitaji mifumo madhubuti ya uchukuzi na usafirishaji inayounganisha bandari, reli, barabara, vituo vya mizigo, viwanda na masoko ili kupunguza vikwazo vya kibiashara na kuongeza ushindani wa bidhaa za Afrika katika masoko ya kimataifa.

Akizungumzia nafasi ya Tanzania, amesema nchi imebarikiwa kuwa na eneo la kimkakati katika Bahari ya Hindi na maziwa makuu, hali inayoipa nafasi ya kuwa kiunganishi muhimu cha biashara kati ya nchi za Afrika Mashariki na Kusini pamoja na masoko ya dunia.

Amesema Bandari ya Dar es Salaam ni lango muhimu la biashara kwa Tanzania na nchi jirani zisizo na mwambao wa bahari, zikiwemo Zambia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Burundi, Rwanda, Malawi na Uganda, hivyo uwekezaji katika miundombinu na huduma za bandari una manufaa kwa ukanda mzima.

Kihenzile amesisitiza kuwa pamoja na uwekezaji katika bandari, meli na miundombinu mingine, nchi za Afrika zinapaswa kuimarisha usalama wa usafiri wa majini, kulinda mazingira ya bahari na maziwa, kutumia teknolojia za kisasa na kuwekeza katika wataalamu wenye ujuzi ili sekta hiyo iweze kuchochea ukuaji wa uchumi na ajira.

Amesema kuanzishwa kwa Chuo Kikuu cha Kikanda cha Usafiri kwa Njia ya Maji kutasaidia kuzalisha wataalamu, kuimarisha utafiti na ubunifu, pamoja na kujenga uwezo wa nchi wanachama kukabiliana na mahitaji yanayoongezeka katika sekta ya usafiri wa majini huku akiongeza kuwa Tanzania ipo tayari kushirikiana na nchi wanachama kuhakikisha chuo hicho kinakuwa kituo cha umahiri kitakachohudumia mahitaji ya kikanda.

Akizungumzia gharama za ujenzi wa chuo hicho Mtendaji Mkuu wa Maritime Organisation for Southern and Northern Africa, Kassim Mpaata, amesema ujenzi wa chuo cha baharini utagharimiwa kwa ushirikiano wa nchi wanachama, huku Serikali ya Tanzania ikiongoza mchakato huo. 

Amesema hatua hiyo inalenga kuimarisha mafunzo ya vijana katika sekta ya bahari na kuendeleza ushirikiano wa nchi hizo.