Wananchi wa Kijiji cha Utende, Wilaya ya Mlele, Mkoa wa Katavi, wametakiwa kuimarisha ushirikiano na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa za uhalifu kwa wakati ili kulinda maisha na mali zao.
Wito huo umetolewa Oktoba 13, 2026 na Polisi kata ya Utende Mkaguzi wa Polisi Kulwa Kusekwa wakati akitoa elimu kwa wananchi wa kijiji hicho, ambapo amewahimiza kuwa mstari wa mbele katika kuzuia uhalifu kwa kutoa taarifa za matukio na viashiria vya uhalifu kwa Jeshi la Polisi.
Aidha, Mkaguzi Kusekwa aliwataka wananchi wenye silaha haramu kuzisalimisha kwa hiari kwa mamlaka husika kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa, akieleza kuwa hatua hiyo itasaidia kupunguza hatari zinazoweza kujitokeza kutokana na matumizi yasiyo halali ya silaha na hivyo kuimarisha usalama wa wananchi na mali zao.
Katika hatua nyingine, wananchi hao wamepewa elimu kuhusu kuchukua tahadhari dhidi ya mvua za El Niño, ikiwemo kuzingatia taarifa na maelekezo yanayotolewa na mamlaka husika, kuepuka maeneo hatarishi yanayoweza kukumbwa na mafuriko na kuchukua hatua za mapema.
