
Afisa Uhusiano wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Getrude Mallya akizungumza na wateja waliotembelea mradi wa Kawe 711, leo Oktoba 13, 2026, jijini Dar es Salaam.


Wafanyakazi wa NHC wakitoa huduma kwa wateja waliotembelea mradi wa Kawe 711


Wateja waliotembelea mradi wa Kawe 711 wakikagua Nyumba za mradi huo
…………..
Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) linaendelea kutoa huduma kwa wateja katika mradi wa Kawe 711 jijini Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Wateja yanayofanyika kuanzia Oktoba 12 hadi 16, 2026.
Akizungumza na wateja waliotembelea mradi huo, leo jijini Dar es Salaam, Afisa Uhusiano wa NHC, Getrude Mallya, amesema maadhimisho hayo ni fursa kwa wananchi kutembelea mradi huo, kujionea ubora wa nyumba za kisasa, kupata taarifa kuhusu mauzo na ushauri wa kitaalamu, pamoja na kufahamu njia mbalimbali za kumiliki nyumba kupitia shirika hilo.
Amesema nyumba zinazojengwa na NHC zimezingatia ubora na mahitaji ya makazi ya kisasa, huku wananchi wakipata fursa ya kuchagua nyumba zinazokidhi mahitaji yao kulingana na uwezo wao.
Aidha, ameeleza kuwa wateja wanaweza kumiliki nyumba kupitia mikopo inayotolewa na benki washirika wa NHC, hatua inayowapa fursa ya kupata makazi kwa utaratibu wa malipo unaozingatia masharti ya mikopo husika.
Mallya ametoa rai kwa wananchi kuchangamkia fursa hiyo kwa kutembelea mradi wa Kawe 711 na kujipatia taarifa sahihi kuhusu upatikanaji wa nyumba, akisisitiza umuhimu wa kutumia fursa zilizopo kumiliki makazi bora na ya kisasa.
Kwa upande wao, baadhi ya wateja waliotembelea mradi huo wameishukuru NHC kwa kuwapa fursa ya kujionea nyumba hizo na kupata maelezo kuhusu ubora wake, huku baadhi yao wakieleza nia ya kununua nyumba baada ya kujiridhisha na huduma na taarifa walizopata.
