Nyumba ya kulala wageni inayojengwa na kikundi cha Juhudi Kijiji cha Likwela Kata ya Nyoni baada ya kupata mkopo kutoka Halmashauri ya wilaya Mbinga

Na Mwandishi wetu,Mbinga

HALMASHAURI ya wilaya Mbinga mkoani Ruvuma,imetoa mikopo kwa vikundi 10 vya wanawake na vijana katika kata ya Nyoni wenye thamani ya Sh.milioni 97.455,500 kutoka kwenye mapato ya ndani kwa ajili ya kuviwezesha vikundi hivyo kiuchumi.

Mratibu wa mikopo kutoka idara ya maendeleo ya jamii ya Halmashauri hiyo Aneth Kiwili alisema, kati ya vikundi hivyo wanawake ni vitatu vilivyopata mkopo wa Sh.23,700,000 na vijana vikundi saba ambavyo vimepata Sh. 73,755,500 ikiwemo kikundi cha Juhudi Sh.milioni 70 kati ya Sh.milioni 107 iliyoomba kwa ajili ya kujenga nyumba ya kulala wageni.

Alisema,ujenzi wa nyumba hiyo utakapokamilika utasaidia kumaliza changamoto ya malazi kwa wageni wanaofika katika kata ya Nyoni kwa shughuli mbalimbali, kutoa ajira kwa vijana na kujiinua kiuchumi kupitia mradi huo.

Aidha Kiwili,amewataka vijana kujiunga kwenye vikundi ili waweze kupata fursa ya mikopo ya asilimia kumi inayotolewa na Halmashauri kwa ajili ya kuanzisha shughuli za kiuchumi badala ya kusubiri kuajiriwa.

Amewasisitiza wana vikundi,kuhakikisha fedha wanazopata zinakwenda moja kwa moja kwenye malengo yaliyokusudiwa ili waweze kunufaika na matunda kupitia miradi wanayoibua na kuepuka matumizi yasiokusudiwa.

Mwenyekiti wa kikundi cha Juhudi kilichopo kijiji cha Likwela Edward Milinga alisema,hadi sasa ujenzi wa mradi huo umefikia hatua ya kufunga milango,madirisha,kuweka malumalu,vitanda,Tv na mahitaji mengine kwa ajili ya wateja.

Hata hivyo,ameiomba Halmashauri kuwapa fedha zilizobaki Sh.37,000,000 ili waweze kukamilisha ujenzi wa mradi huo ambao utasaidia kupunguza changamoto ya malazi kwa wageni wataofika katika kata ya Nyoni kwa ajili ya shughuli mbalimbali ikiwemo biashara.

Naye mwanachama wa kikundi hicho Steven Milinga alisema,walianza ujenzi wa mradi huo mwaka 2025 lakini ujenzi wake umesimama kutokana na kukosa fedha za umaliziaji.

Alisema,katika mradi huo kutakuwa na huduma ya vinywaji na chakula ili kuongeza mapato yatakayowezesha kuingiza fedha na hatimaye waweze kurudisha mkopo waliochukua kwa wakati.

Ameishukuru Halmashauri ya wilaya Mbinga,kuwapa mkopo huo ambao utawasaidia kuwapa fedha hivyo kujikwamua kiuchumi na kutoa ajira kwa baadhi ya vijana wengine wa kijiji cha Likwela na kata ya Nyoni kwa ujumla.