Na Mwandishi wetu, Simanjiro
NAIBU Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, James Kinyasi Ole Millya amewataka wakazi wa Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, kutobeza uteuzi uliofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan ila kushukuru na kupokea.
Ole Millya ambaye pia ni Mbunge wa Simanjiro ameeleza hayo kwenye ziara yake iliyofanyika kijiji cha Kimotorok kata ya Loiborsiret ya kuzungumza na wananchi, kuwashukuru na kusikiliza kero zao.
Amesema wilaya ya Simanjiro tangu ianzishwe haijawahi kupata kiongozi ngazi ya Naibu Waziri hivyo haipaswi kubezwa zaidi ya kushukuru mamlaka ya uteuzi.
“Wana Simanjiro tukipata nafasi ya uteuzi hata kama ni ndogo tunapaswa kushukuru kwa moyo mkunjufu na siyo kuibeza,” amesema Ole Millya.
Diwani wa kata ya Komolo, Saning’o Somii amesema baadhi ya viongozi wastaafu wanapotosha jamii kuwa nafasi ya Naibu Waziri ni ndogo kuliko mkuu wa mkoa waliowahi kushikilia.
“Mtu badala ya kukaa pembeni baada ya kukosa uongozi anataka kwenye sherehe aimbiwe wimbo wa sifa kama yupo madarakani,” amesema Somii.
Diwani wa kata ya Terrat, Jackson Ole Materi amesema wastaafu wanaowashwa watulie waache viongozi waliochaguliwa wafanye kazi.
“Mtu anasema yeye alikuwa mkuu wa mkoa ni nafasi kubwa kuliko nafasi ya Naibu Waziri jambo ambalo siyo sahihi kwani Naibu anazunguka nchi nzima na mkuu wa mkoa anaongoza mkoa mmoja, pia Naibu anakuwepo kwenye Baraza la Mawaziri tofauti na RC,” amesema Ole Materi.
Mkazi wa kijiji cha Kimotorok, Nai Mollel amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kumteua Ole Millya kushika nafasi hiyo ya Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
“Ningemuona mama yetu Samia ningemkumbatia na kumbusu mara 10 kama ishara ya kumshukuru kwa kumteua kuwa Naibu Waziri mtoto wetu Ole Millya,” amesema Nai.
Katibu wa CCM Wilaya ya Simanjiro Wambura Igembya amewataka wana Loiborsiret kuacha siasa ambazo siyo za kistaarabu na kusimama kwenye maendeleo.
Diwani wa Loiborsiret, Ezekia Lesenga (Mardadi) amemshukuru Ole Millya kwa namna anavyoshughulikia migogoro ya ardhi Simanjiro.
Mardadi amesema kipindi cha kwanza cha ubunge wa Ole Millya mwaka 2015/2020 alisababisha Mawaziri nane kufika kwenye kata hiyo ili kutatua migogoro.
