Na. Meleka Kulwa-Fullshangwe Blog,Dodoma
Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), Dkt. Bill Kiwia, amesisitiza umuhimu wa ushirikiano na Wathibiti Ubora wa Elimu katika ukusanyaji na uhakiki wa taarifa sahihi za wanafunzi ili kuhakikisha mikopo inatolewa kwa wakati na kuwafikia walengwa.
Ameyasema hayo Oktoba 9, 2026, Jijini Dodoma wakati wa kikao kazi kati ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia (WyEST), HESLB na Wathibiti Ubora wa Elimu kutoka mikoa yote 26 ya Tanzania Bara, kilicholenga kuimarisha ushirikiano katika upatikanaji wa taarifa za wanafunzi wanaohitaji mikopo ya elimu ya juu.
Amesema taarifa sahihi kuhusu matokeo ya mitihani, wanafunzi yatima, wenye ulemavu na wenye mahitaji maalumu ni muhimu katika kupanga bajeti, kugawa fedha za mikopo na kuishauri Serikali kuhusu mahitaji halisi ya utoaji wa mikopo ya elimu ya juu.
Aidha, amebainisha kuwa matumizi ya mifumo ya taarifa iliyopo katika taasisi mbalimbali yatasaidia kupata na kuhakiki taarifa kwa haraka, kupunguza makosa na taarifa za kughushi, pamoja na kuondoa usumbufu kwa wanafunzi wanaoomba mikopo.
Ameongeza kuwa ushirikiano huo utasaidia kuhakikisha taarifa zinazowasilishwa HESLB zinatoka katika mamlaka husika na kuthibitishwa ipasavyo, hususan taarifa zinazohusu hali za wanafunzi ili mikopo itolewe kwa kuzingatia mahitaji halisi ya walengwa.
Amebainisha Kuwa upatikanaji wa taarifa kwa wakati ni muhimu katika kuhakikisha wanafunzi wanapata mikopo au fedha zao kwa wakati wanaporipoti katika vyuo vyao, huku akisisitiza umuhimu wa mifumo ya taasisi mbalimbali kusomana ili kurahisisha upatikanaji wa taarifa.
Amesema Serikali imetenga shilingi bilioni 787.4 kwa ajili ya mikopo na msaada wa wanafunzi katika mwaka huu, ambapo zaidi ya wanafunzi 292,400 wanatarajiwa kunufaika, wakiwemo wanafunzi wapya zaidi ya 81,300, wanafunzi 160,738 wanaoendelea na masomo na zaidi ya wanafunzi 11,000 wa ngazi ya stashahada.
Ameongeza kuwa ongezeko la wanafunzi wanaotarajiwa kunufaika na mikopo linaonesha umuhimu wa kuwa na taarifa sahihi na zilizohakikiwa ili kuwezesha upangaji na usimamizi wa rasilimali zinazotengwa kwa ajili ya elimu ya juu.
Awali, Mkurugenzi wa Uthibiti Ubora wa Shule wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Ephraim Simbeye, amesisitiza umuhimu wa ushirikiano katika kuhakikisha taarifa za wanafunzi zinakusanywa na kuhakikiwa kwa usahihi ili kuimarisha utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wanaostahili.
Katika kikao hicho, wito umetolewa kwa viongozi na mamlaka zinazohusika kushirikiana katika ukusanyaji, uhakiki na uwasilishaji wa taarifa kwa wakati, ili kuimarisha uwazi na kuhakikisha mikopo ya elimu ya juu inawanufaisha wanafunzi wanaostahili.

