Na. Veronica Mwafisi-Moshi
07 Oktoba, 2026.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete amewataka Watumishi wa Umma waliokuwa katika michezo ya SHIMIWI watakaporudi katika maeneo yao ya kazi, kufanya kazi kwa kusimamia mifumo ya utekelezaji wa majukumu mbalimbali waliyokasimiwa ikiwemo ujazaji wa Mfumo wa Upimaji wa Utendaji kazi (PEPMIS).

Waziri Kikwete amezungumza hayo leo tarehe 07 Oktoba, 2026 wakati akihitimisha rasmi michezo ya SHIMIWI iliyofanyika katika Mkoa wa Kilimanjaro.
“Nitoe wito kwenu watumishi wenzangu, leo tunapohitimisha rasmi michezo hii ya SHIMIWI, mtakaporudi katika maeneo yenu ya kazi hakikisheni mnasimamia Mifumo ya utekelezaji wa majukumu yenu ikiwemo ujazaji wa PEPMIS,” amesema Mhe. Kikwete
Waziri Kikwete amesema, taasisi zote za Serikali zina utaratibu mzuri wa kumpima kila mtumishi kiutendaji hivyo, mafanikio ya mtu mmoja mmoja, Idara na taasisi kwa ujumla yatasaidia kujua utendaji wa Serikali nzima.
Ameongeza kuwa, ni vema kujenga ushirikiano kwa washiriki wa michezo hiyo ya SHIMIWI ambao utawasaidia katika utekelezaji wa majukumu mbalimbali katika maeneo yao ya kazi.
“Mkusanyiko huu mkubwa wa Watumishi wa Umma unatusaidia kuwa na uelewa wa masuala mbalimbali pamoja na kujenga ushirikiano utakaoleta mafanikio kwenye maeneo yenu ya kazi,” ameongeza Mhe. Kikwete
Aidha, Mhe. Ridhiwani amesisitiza suala la usimamizi wa Rasilimalifedha kwa Viongozi wa Klabu mbalimbali na kutaka kila ofisi kutenga bajeti kwa ajili ya mipango ya mwaka unaofuata.
Akihitimisha hotuba yake, Mhe. Ridhiwani amesema kutokana na Kaulimbiu ya SHIMIWI 2026, inayosema Watumishi Tupo Tayari kwa AFCON 2027, kila mtumishi katika sekta aliyopo ahakikishe anaunga mkono mashindano hayo kwa ustawi wa Taifa letu.
