NA DENIS MLOWE IRINGA

JESHI la Polisi Mkoa wa Iringa limeendelea na kampeni ya ‘Ongea na Kamanda’ kwa kuwafikia wananchi katika maeneo yao, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kusikiliza changamoto zao, maoni na ushauri kuhusu masuala ya usalama.

Kampeni hiyo imeanza katika eneo la Njiapanda ya Nyololo, Wilaya ya Mufindi, mkoani Iringa, ambapo wananchi walipata fursa ya kuwasilisha hoja na kero mbalimbali zinazohusiana na usalama katika maeneo yao.

Akizungumza katika kampeni hiyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, SACP Allan Bukumbi, amesema Jeshi la Polisi litaendelea kuwafikia wananchi katika maeneo ya makazi na biashara ili kusikiliza changamoto zao na kupata maoni yatakayosaidia kuboresha huduma zinazotolewa na jeshi hilo.

Amesema ushirikiano kati ya Jeshi la Polisi na wananchi ni muhimu katika kuzuia uhalifu, hivyo wananchi wanapaswa kutumia fursa zinazotolewa kupitia kampeni hiyo kueleza changamoto wanazokutana nazo na kutoa taarifa zinazohusiana na usalama.

Kwa upande wao, wakazi wa Kata ya Nyololo wamepongeza kampeni hiyo wakisema imewapa nafasi ya kuzungumza moja kwa moja na viongozi wa Jeshi la Polisi kuhusu masuala yanayowahusu katika maeneo yao.

Wamesema kupitia kampeni hiyo wameweza kupata ufafanuzi wa baadhi ya masuala ya kiusalama pamoja na kueleza changamoto wanazokutana nazo, hali ambayo wameeleza kuwa inasaidia kujenga uhusiano mzuri kati ya wananchi na Jeshi la Polisi.

Wananchi hao wameahidi kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa za uhalifu na matukio mengine yanayoweza kuhatarisha usalama, huku wakisisitiza umuhimu wa kampeni hiyo kuendelea katika maeneo mbalimbali.