Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imeendelea kuwa kiungo muhimu katika kuwezesha waendelezaji wadogo wa miradi ya uzalishaji wa umeme unaotokana na maporomoko ya maji, hatua inayolenga kuongeza upatikanaji wa umeme nchini na kuhakikisha wananchi wanapata nishati ya uhakika kwa ajili ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Nishati Jadidifu na Teknolojia Mbadala wa REA, Mhandisi Advera Mwijage, wakati akitembelea na kukagua maendeleo ya mradi wa kuzalisha umeme kwa maporomoko ya maji katika kijiji cha Boimanda wilayani Ludewa, mkoani Njombe.
Mradi huo una uwezo wa kuzalisha Kilowati 317 za umeme na unasimamiwa na Shirika la Masista wa Benedictine wa Kanisa Katoliki.
Mhandisi Mwijage amesema Serikali kupitia REA imetoa zaidi ya shilingi milioni 738 katika awamu ya pili kwa ajili ya kuendeleza mradi huo, huku sehemu kubwa ya miundombinu ikiwa tayari imekamilika.
Kwa mujibu wa Mhandisi Mwijage, jengo la kuhifadhia mitambo ya kuzalisha umeme limekamalika na kinachobaki ni kukamilisha miundombinu ya kusafirisha umeme kutoka katika mradi huo hadi kwenye mfumo wa TANESCO, ili umeme unaozalishwa uweze kuingizwa katika gridi ya taifa.
Aidha, Mhandisi Mwijage amewataka wananchi wanaoishi katika maeneo yanayozunguka mradi huo kuendelea kutunza mazingira na kulinda vyanzo vya maji, akisema upatikanaji wa maji ya kutosha ni muhimu kwa uendelevu wa mradi huo.
Kwa upande wake, Sister Imakulata Mlowe msimamizi wa mradi huo kutoka Shirika la Benedictine Sisters la Kanisa Katoliki, ameishukuru Serikali kupitia REA kwa kuwezesha mradi huo, akisema hadi sasa wamepokea zaidi ya shilingi bilioni 4.5 kwa ajili ya ujenzi na maendeleo ya mradi huo.
Amesema fedha hizo zimetumika katika ujenzi wa bwawa, jengo la kufulia umeme maarufu kama power house, pamoja na miundombinu ya kusafirisha umeme kwa wananchi wa Vijiji vya Boimanda na Matola.
Amesema mradi huo ukikamilika utakuwa na mchango mkubwa katika kuboresha maisha ya wananchi, kuongeza shughuli za kiuchumi na kurahisisha upatikanaji wa huduma mbalimbali zinazohitaji umeme.
Ametaja baadhi ya manufaa kuwa ni pamoja na wananchi kupata mwanga wa uhakika, kuanzisha na kuendesha shughuli ndogo za biashara, huduma za maji, saluni na matumizi ya mashine mbalimbali, pamoja na kuboresha huduma za afya.
Mradi huo ni miongoni mwa juhudi za Serikali za kuongeza uzalishaji wa umeme kupitia vyanzo vya nishati jadidifu, huku ushiriki wa sekta binafsi ukitarajiwa kuongeza kasi ya upatikanaji wa umeme katika maeneo ya vijijini na kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

