Kyerwa. Mbunge wa Jimbo la Kyerwa, Mhe. Khalid Mussa Nsekela, amekutanisha mameneja wa taasisi mbalimbali zinazotoa huduma muhimu wilayani humo katika kikao maalum cha kujadili hali ya miundombinu na changamoto zinazowakabili wananchi wa jimbo hilo.

Kikao hicho kilichofanyika katika Ofisi ya Mbunge kiliwakutanisha mameneja wa TARURA, RUWASA, TANESCO, TANROADS pamoja na taasisi nyingine zinazohusika na huduma za msingi, ambapo pamoja na mambo mengine walijadili hali ya barabara, upatikanaji wa maji, umeme na huduma nyingine muhimu kwa wananchi.

Mhe. Nsekela amesema kikao hicho kililenga kupata uelewa wa kina kuhusu changamoto zilizopo katika maeneo mbalimbali ya Jimbo la Kyerwa na kubaini zile zinazohitaji ufumbuzi wa haraka. 

Amesema miundombinu bora ni muhimu kwa shughuli za kiuchumi na kijamii, hivyo viongozi wa taasisi hizo wanapaswa kuhakikisha wanakuwa karibu na wananchi.

Aidha, Mbunge huyo amewataka mameneja hao kuhakikisha changamoto ambazo zinaweza kutatuliwa katika ngazi zao zinafanyiwa kazi kwa wakati, huku zile zilizo nje ya uwezo wa taasisi zao zikifikishwa katika mamlaka husika kwa ajili ya hatua zaidi.

Mhe. Nsekela amesema kikao hicho pia ni sehemu ya ufuatiliaji wa utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2025–2030, hususan katika maeneo ya huduma za kijamii na miundombinu. Kwa upande wao, mameneja hao wamemshukuru Mbunge huyo kwa kuwaunganisha na kuweka utaratibu wa pamoja wa kufuatilia changamoto za huduma katika Wilaya ya Kyerwa.