­▫️Umuhimu wa Uwazi na Uwajibikaji katika usimamizi wa Rasilimali Madini, Mafuta na Gesi Asilia wasisitizwa

▫️Umuhimu wa Mashirikiano ya Kimataifa wasisitizwa

▫️Tanzania kufanyiwa Tathimini ya utekelezaji wa shughuli za EITI Julai, 2027

📍Brussels, Belgium 🇧🇪 

Leo tarehe 8 Oktoba, Mkutano Mkuu wa Kimataifa wa EITI ( EITI Global Conference 2026) umefunguliwa Rasmi. Mkutano huu umekutanisha nchi zaidi ya 57 zinazotekeleza Matakwa ya Kimataifa ya EITI ambapo mada mbalimbali zimejadaliwa ili kuimarisha uelewa wa utekelezaji wa vigezo vya Kimataifa ya EITI. Mkutano huu pia ni fursa ya kubadilishana uzoefu wa namna bora ya usimamizi wa rasilimali Madini, Mafuta na Gesi Asilia.

Akifungua Mkutano huu, Mwenyekiti wa Bodi ya Kimataifa wa EITI anayemaliza muda wake Rt. Helen Clark amesisitiza umuhimu wa Mashirikiano kati ya Serikali, Kampuni za Madini, Mafuta na Gesi Asilia na Asasi za Kiraia. Amesema ni muhimu kushirikiana kikamilifu ili kuhakikisha rasilimali zetu duniani zinanufaisha nchi zetu na wananchi wote kwa ujumla.

Rt. Helen, ameongoza bodi ya Asasi ya Kimataifa ya EITI kwa kipindi cha miaka saba(7) na amefanikiwa kuhakikisha kila nchi wanachama wa EITI wanatekeleza majukumu yao kikamilifu ili kuhakikisha uwazi na uwajibikaji unaongezeka katika usimamizi wa rasilimali hizi muhimu.

Nae, Mwenyekiti mpya wa Asasi ya Kimataifa ya EITI – Maria Van Der Hoeven ameahidi kutoa ushirikiano kwa nchi wanachama wa Asasi ya EITI katika kusimamia utekelezaji wa vigezo vya Kimataifa vya EITI kwa ukubwa wake. Mwenyekiti Mpya wa EITI ataongoza Bodi ya EITI kuanzia mwaka 2026 hadi 2029.Kwa upande mwingine, Mwenyekiti wa Kamati ya TEITI Balozi Wilson Masilingi amefanya Mkutano na Katibu Mtendaji wa Asasi ya EITI Bw. Mark Robinson ambapo, Katibu Mtendaji huyo ameridhishwa na Tanzania katika Utekelezaji wa Shughuli za EITI na kupongeza jitihada mbalimbali ambazo Kamati ya TEITI inafanya katika kuhakikisha shughuli zinafanyika kulingana na Matakwa ya EITI. Pia, Tanzania imepongezwa kwa jitihada zinazofanywa hasa kwa kutumia wataalam wa ndani katika kuandaa ripoti za TEITI za kila mwaka.

Sambamba na Mkutano unaoendelea, Tanzania kama nchi mwanachama wa EITI imeshiriki katika maonesho mbalimbali ambapo nchi wanachama wa EITI wamepata fursa ya kuonesha bidhaa na huduma wanazofanya kutekeleza masuala ya uwazi na uwajibikaji katika sekta ya uziduaji.

Mkutano Mkuu wa Asasi ya Kimataifa utahitimishwa tarehe 9 Oktoba, 2026 huku Mada mbalimbali zimeendelea kujadiliwa kwa lengo la kujengeana uzoefu katika utekelezaji wa shughuli za Uwazi na Uwajibukaji katika usimamizi wa Rasilimali Madini, mafuta na gesi asilia duniani.