Na Ripota wa TBN, Arusha. 

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), Mhe. Anda Filip, ameipongeza Tanzania kwa hatua iliyopiga katika kuongeza idadi ya ushiriki wa wanawake katika siasa na uongozi, na kueleza kuwa uzoefu wa Tanzania unaweza kuwa somo kwa mataifa mengine katika kujenga mifumo jumuishi ya kufanya maamuzi.

Akizungumza katika mahojiano maalumu yaliyofanyika Oktoba 7, 2026 wakati wa Mkutano wa 153 wa IPU unaofanyika Arusha, Filip amesema anavutiwa na namna Tanzania ilivyoongeza idadi uwakilishi wa wanawake katika Bunge la Jamhurin ya Muungano wa Tanzania, ambao kwa sasa umefikia zaidi ya asilimia 39.

Katika mkutano huo, Mhe. Filip amesisitiza kuhusu umuhimu wa kuhakikisha wanawake wanapata nafasi ya kushiriki kikamilifu katika michakato ya kisiasa na maamuzi ya kitaifa.

Filip amesema kupitia Dira ya Maendeleo 2050, Tanzani ina fursa ya kuimarisha ushiriki wa wanawake na vijana katika kujenga na kutekeleza ajenda za maendeleo ya muda mrefu, ili kuhakikisha vipaumbele vya taifa vinaendelea kutekelezwa na vizazi vijavyo bila kutegemea mabadiliko ya awamu za uongozi.

Katika mkutano wa IPU unaendelea jijini Arusha, Tanzania inawakilishwa na Wabunge nane ambapo kati ya hao, Wabunge wanne ni wananwake ikiwa ni sawa na asilimia 62.5 ya uwakilishi wa wanawake wanaoiwakilisha Tanzania katika Umoja wa Mabunge Duniani (IPU).

Wabunge hao wanawake ni Mheshimiwa Dkt. Pindi Chana, Mheshimiwa Dkt. Zeyana Hamid, Mheshimiwa Kiza Myeye, Mheshimiwa Mhandisi Fatma Rembo na Mhehimiwa Asha Feruzi. 

Wabunge wengine waliopo IPU ambao ni wanaume ni Mheshimiwa. Dkt. Damas Ndumbaro, Mheshimiwa Elibariki Kingu na Mheshimiwa Rashid Shangazi, ambao idadi yao ni sawa na asilimia 37.2 ya uwakilishi wa wabunge wa Tanzania.

Mkutano wa 153 wa Umoja wa Mabunge Duniani ulianza tarehe 5 Oktoba, 2026 katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC) na unatarajia kuhitimishwa Ijumaa Oktoba 9, 2026. Mkutano huu umeshirikisha wajumbe zaidi ya 2000 kutoka mataifa mbalimbali.