Shirika la Foundation for Disabilities Hope (FDH) Tanzania limeanza kuchukua hatua za kuwasaidia watu wenye ulemavu na familia zao kukabiliana na athari zinazoweza kujitokeza kutokana na mvua za El Niño zinazotarajiwa nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mkurugenzi Mtendaji wa FDH Tanzania, Maiko Salali, amesema watu wenye ulemavu ni miongoni mwa makundi yaliyo katika hatari kubwa zaidi wakati wa majanga, hivyo shirika hilo limeanza kutambua familia zenye uhitaji mkubwa na kuzipatia msaada wa chakula na mahitaji muhimu.
Amesema hatua hiyo inalenga kuhakikisha watu wenye ulemavu ambao familia zao hazina uwezo wa kutosha wa kununua na kuhifadhi chakula wanakuwa salama katika kipindi hiki ambacho mamlaka zimetoa tahadhari kuhusu mvua hizo.
“Tunachukua jitihada ya kwanza kutathmini familia ambazo tunadhani zina changamoto kubwa au zina mahitaji makubwa na kuweza kuzipelekea msaada huu wa vyakula na mahitaji mbalimbali,” amesema Salali.
Amesema FDH inalenga kufikisha msaada huo kwa zaidi ya kaya 150 za watu wenye ulemavu, huku akitoa wito kwa wadau, taasisi na mashirika mengine kushirikiana na FDH pamoja na Serikali kuhakikisha kundi hilo linapata ulinzi na msaada unaohitajika wakati wa majanga.
Salali pia amewataka watu wenye ulemavu, wazazi, walezi na jamii kwa ujumla kuchukua tahadhari dhidi ya athari zinazoweza kusababishwa na mvua hizo, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha chakula kinahifadhiwa vizuri, kukaa katika maeneo salama na kusafisha mazingira yanayoweza kuhatarisha usalama wao.
Amesema FDH itaendelea kutoa taarifa na kuwaelimisha watu wenye ulemavu kuhusu namna ya kuchukua tahadhari ili kupunguza madhara yanayoweza kujitokeza.
“Tunafahamu changamoto za watu wenye ulemavu ni kubwa. Kwa hiyo tunaomba familia, wazazi, walezi na jamii inayowazunguka watu wenye ulemavu kuwasaidia kuchukua tahadhari ili tuweze kukabiliana na janga hili na tahadhari zilizotolewa kuhusu mvua za El Niño,” amesema.
Kwa upande wake, Meneja Mahusiano wa FDH Tanzania, Godfrey Mpunza, amesema tahadhari iliyotolewa na mamlaka inapaswa kuwa kichocheo kwa jamii kuanza maandalizi mapema badala ya kusubiri madhara yatokee.
“Maana yake ni kwamba tunapaswa kuanza kujiandaa mapema dhidi ya janga linalotarajiwa kutokea, kama ambavyo mamlaka husika zimeeleza. Sisi kama FDH tumeanza kuchukua hatua za maandalizi na kuwafikia watu wenye ulemavu wenye uhitaji,” amesema Mpunza.
Amesema maandalizi hayo ni muhimu kwa sababu watu wenye ulemavu wanaweza kukumbana na changamoto zaidi wakati wa majanga, hivyo hatua za mapema zinahitajika ili kuhakikisha wanapata taarifa, msaada na mazingira salama.
Mpunza ametoa wito kwa wadau wengine, mashirika na taasisi mbalimbali kushirikiana na FDH pamoja na Serikali katika kuhakikisha maandalizi yanafanyika kwa pamoja ili kupunguza athari za mvua hizo.
“Tunatoa wito pia kwa wadau wengine tushirikiane nasi ili kwa pamoja tuweze kukabiliana na athari zinazoweza kusababishwa na mvua za El Niño na kuhakikisha kundi la watu wenye ulemavu linakuwa salama,” amesema.
FDH imesisitiza umuhimu wa familia za watu wenye ulemavu kuchukua tahadhari mapema, ikiwemo kuhifadhi chakula, kusafisha mazingira, kuepuka maeneo hatarishi na kuhakikisha watu wenye ulemavu wanapata taarifa muhimu kuhusu tahadhari zinazotolewa na mamlaka.

