Meneja wa EWURA Kanda ya Ziwa Nyirabu Musira akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) katika maadhimisho ya wiki ya Huduma kwa Wateja
…………
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imewahimiza wananchi kuwekeza kwenye vituo vya mafuta katika maeneo ya vijijini kutokana na Serikali kupunguza gharama za leseni kwaajili ya kurahisisha uwekezaji.
Hayo yamebainishwa na Meneja wa EWURA Kanda ya Ziwa, Nyirabu Musira alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kwenye banda lao lililoko nje ya ofisi yao katika wiki ya Huduma kwa Wateja.
Amesema Serikali imerahisisha masharti ya uwekezaji wahuduma za vituo vya mafuta vijijini ambapo kwa shilingi 50,000 unaweza kuomba leseni na shilingi 100,000 ni kwaajili ya kulipia leseneni kwa kipindi chote cha miaka mitano.
“Leseni ya kawaida kwa maeneo ya mjini inagharimu shilingi 500,000 kwenye maombi ya leseni na shilingi milioni moja kwaajili ya kulipia leseni kwa kipindi cha miaka mitano hivyo gharama za vijijini zimerahisishwa sana ukilinganisha na mjini”,
Amesema kwa wale wanaofanya huduma za ufungaji wa miundombinu ya umeme kwenye majumba au maeneo mbalimbali wanapaswa kuwa na leseni za EWURA.
“Uwepo wa watu wanaoshughulika na huduma tunazozidhibiti pasipo kuwa na leseni ni kosa kisheria na inaweza kusababisha changamoto kubwa ikiwemo kuhatarisha watu na mali zao”, Amesema Musira
Aidha, amesema kwenye wiki hiyo ya Huduma kwa Wateja imeonekana watu hawana uelewa juu ya haki zao pale wanapohitaji huduma hivyo EWURA inajukumu la kuendelea kutoa elimu zaidi ili wananchi wajue kuwa kunamikataba ya huduma kwa wateja ambayo wanatakiwa waifahamu kama wateja pamoja na haki zilizomo.
“Mfano moja ya haki ambayo tumekuwa tukiielezea katika kipindi hiki cha wiki ya Huduma kwa Wateja ni haki ya kuunganishiwa huduma ndani ya muda ambao mtoa huduma ameusema kwenye mkataba,na haki hiyo inampa mpokeaji wa huduma haki ya kupata fidia endapo itatokea hajapata huduma kwa muda uliotajwa kwenye mkataba wa huduma kwa wateja”,
