Kampuni ya ndege ya British Airways imetangaza kurejesha safari za moja kwa moja kati ya Uingereza na Tanzania kuanzia Mei 2027, hatua inayolenga kuongeza usafiri wa watalii na wasafiri wa kibiashara kati ya mataifa hayo.
Tangazo hilo limetolewa Oktoba 7, 2026, na Mkuu wa Masoko wa British Airways kwa Bara la Afrika, Asia na Pasifiki, Bw. Moran Birger, katika Jukwaa la Uwekezaji kati ya Tanzania na Uingereza, katika ukumbi wa Mikutano wa Peninsula Hotel London Uingereza. Jukwaa hilo limefunguliwa na Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba
Birger amesema uamuzi huo umechangiwa kwa kiasi kikubwa na kuongezeka kwa idadi ya wasafiri na watalii wanaoitembelea Tanzania, sambamba na maendeleo ya kiuchumi na uwekezaji ambayo yameifanya Tanzania kuvutia watu wengi kufanya uwekezaji.
Kwa Upande wake Dkt. Mwigulu amepongeza uamuzi huo akiutaja kuwa utasaidia kwa kiasi kikubwa kuendelea kuifungua Tanzania na kuwa kichocheo kikubwa cha uchumi kwa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.
Kadhalika, Dkt. Dkt Mwigulu amesema Tanzania ni kitovu cha uwekezaji na ina masoko zaidi. “Kwa mwekezaji anayataka kuja kuwekeza Tanzania, asiangalie soko la ndani tu, bali aione Tanzania kama jukwaa la kuwafikia wadau wengi wa kikanda kwani inanknda nyingi inazojihusisha nazo,” amesema.
Amewaambia washiriki wa Kongamano hilo wapatao 300 kwamba amani, utulivu na uongozi imara usiotetereka ndiyo mtaji mkubwa wa kuifanya Tanzania kuwa jukwaa la uwekezaji.
Mbali na hayo, Waziri Mkuu amesema uwepo wa umeme wa uhakika, miundombinu ya barabara, reli ya kisasa ya SGR, bandari na viwanja vya ndege ni vichocheo vikubwa vya kuharakisha maendeleo nchini.
Amesema mageuzi ya kiuchumi ambayo Tanzania imeyapanga kulingana na DIRA 2050, yanataka uwepo wa umeme wa uhakika na wa bei nafuu.
Kwa upande wake Waziri Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji Kitila Mkumbo, amesema, Serikali ya Awamu ya Sita imeandaa Dira ambayo inafungua njia na muelekeo wa nchi.
“Nchi imeandaa sera, mipango na malengo thabiti kufanikisha malengo yake na kuwezesha ukuaji wa uchumi kwa mwananchi mmoja mmoja na ukuaji wa uchumi wa nchi kwa ujumla”

