Na Sophia Kingimali, Dar es Salaam
Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Reuben Kwagilwa, amesema serikali, sekta binafsi, taasisi za fedha, watafiti, wabunifu, wajasiriamali na washirika wa maendeleo wanapaswa kushirikiana kufungua fursa za uwekezaji na biashara katika uchumi wa buluu.
Kwagilwa ametoa wito huo leo Octoba 7,2026 wakati wa Jukwaa la Biashara kuhusu kufungua fursa za uwekezaji na biashara kwa ajili ya uchumi endelevu wa buluu katika Bahari ya Hindi ya Magharibi.
Kwagilwa amesema ushirikiano huo ni muhimu katika kubadilisha uwezo wa uchumi wa buluu kuwa fursa endelevu za biashara na uwekezaji, huku akisisitiza umuhimu wa kuunganisha uongozi wa bahari, uhifadhi, biashara na uwekezaji.
Amesema Tanzania ina maeneo mbalimbali ya kuangazia katika uwekezaji kwenye Bahari ya Hindi, yakiwemo nishati, uvuvi, usafirishaji, utalii na michezo, pamoja na kilimo cha mwani na shughuli nyingine zinazohusiana na rasilimali za bahari.
“Tunataka kuangazia fursa zote zilizopo kwenye Bahari yetu ya Hindi: fursa kwenye maeneo ya nishati, fursa kwenye maeneo ya uvuvi, fursa kwenye maeneo ya usafirishaji, fursa kwenye maeneo ya utalii pamoja na michezo,” amesema.
Amesema shughuli nyingine zinazoweza kuchochea uchumi wa buluu ni uchimbaji wa madini na utafutaji wa nishati baharini, ambazo kwa pamoja zinaunda mnyororo mpana wa shughuli za kiuchumi unaohitaji uwekezaji na usimamizi endelevu.
Kwagilwa amesisitiza kuwa nchi wanachama wa Mkataba wa Nairobi zinapaswa kuendelea kushirikiana katika kuhifadhi bahari na kutumia kwa pamoja fursa za uchumi wa buluu, kwa kuwa mifumo ya ikolojia ya bahari na rasilimali zake haifuati mipaka ya kiutawala ya nchi moja.
Amesema mjadala huo umefanyika katika siku ya pili ya Mkutano wa 12 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Nairobi (COP12) unaoendelea jijini Dar es Salaam, ukiwakutanisha wafanyabiashara, wajasiriamali, taasisi za fedha, watafiti, taasisi za elimu ya juu na wavumbuzi kujadili namna ya kuunganisha fursa za bahari na biashara, fedha na masoko.
UKANDA wa Magharibi mwa Bahari ya Hindi umetakiwa kubadili mtazamo wa uchumi wa buluu kwa kuacha kuzungumzia zaidi wingi wa rasilimali zilizopo na badala yake kuzigeuza kuwa biashara endelevu zinazowekezeka na kuongeza thamani ya maliasili.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Maendeleo na Uratibu wa Uchumi Buluu, Wizara ya Uchumi Buluu na Uvuvi Zanzibar, Mondy Muhando, amesema changamoto kubwa kwa sasa si kugundua rasilimali na fursa zilizopo katika ukanda huo, bali ni namna ya kuzibadilisha kuwa biashara zinazoweza kuvutia uwekezaji, kuongeza thamani na kuleta manufaa ya kiuchumi.
Amesema ukanda huo una utajiri mkubwa wa maliasili ikiwemo mwani, uvuvi, matumbawe, mikoko, bandari, utalii na njia za kimkakati za usafiri wa baharini, lakini rasilimali hizo zinahitaji kuunganishwa na mifumo ya biashara ili ziwe na tija zaidi.
“Kwa hiyo, changamoto yetu si kugundua kile tulicho nacho au uwezo tulio nao. Badala yake, changamoto yetu ni jinsi gani tutabadilisha vyote tulivyo navyo kuwa biashara endelevu na zinazowekezeka,” amesema.
Amesema mwekezaji haangalii rasilimali pekee, bali huzingatia pia masoko, miundombinu, vibali, vihatarishi na faida inayoweza kupatikana, hivyo ni muhimu kujenga mazingira yanayowezesha rasilimali hizo kuunda mnyororo wa thamani.
