Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Juma Mkomi akizungumza na Maafisa Rasilimaliwatu na Wahasibu kutoka Wizara na Taasisi za Umma Mkoa wa Dodoma kwenye Mafunzo kuhusu taratibu za kuwasilisha na kushughulikia madai ya fidia kwa wafanyakazi yaliyofanyika Oktoba 7, 2026 katika ukumbi wa LAPF Jijini Dodoma.
Na. Antonia Mbwambo – Dodoma
Tarehe 7 Oktoba, 2026
Uzembe na ucheleweshaji wa taarifa unaofanywa na baadhi ya Maafisa Rasilimaliwatu Serikalini unaathiri mchakato wa kushughulikia madai ya fidia kwa mfanyakazi wakati anapopata ajali, ugonjwa au kifo anapokuwa katika utekelezaji wa makumu ya kikazi.
Maneno hayo yalisemwa na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma Bw. Juma Mkomi Oktoba 7, 2026 wakati akifungua mafunzo yaliyoandaliwa na Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) kwa Maafisa Rasilimaliwatu na Wahasibu wa Wizara, Taasisi za Umma zilizopo Dodoma na Wilaya zote za Mkoa Dodoma kuhusu taratibu za kuwasilisha na kushughulikia madai ya fidia kwa wafanyakazi yaliyofanyika katika ukumbi wa LAPF Jijini Dodoma.
Bw. Mkomi alisema kuwa hapendi kuona mfanyakazi kwa bahati mbaya anapata ajali au ugonjwa unaotokana na kazi lakini kutokana na kutokuwepo kwa taarifa sahihi, nyaraka muhimu au uelewa wa taratibu, anashindwa kupata haki yake kwa wakati.
“Mafunzo haya ni muhimu kwenu Maafisa Rasilimaliwatu kwa kuwa ndio kiungo kati ya mwajiri, mfanyakazi na mifumo mbalimbali inayohusika na usimamizi wa rasilimaliwatu, ninaamini baada ya mafunzo haya mtakuwa na uelewa wa hatua za kuchukua pale mfanyakazi anapopata ajali au ugonjwa unaotokana na kazi au anapofariki kutokana na mazingira yanayohusiana na kazi na kuharakisha upatikanaji wa fidia” alisema Bw. Mkomi.
Aliongeza kuwa, kuwasilisha taarifa sahihi, zenye ukamilifu na kwa wakati ni jambo muhimu katika mchakato wa fidia. Hivyo, mafunzo hayo ni muhimu kwa kuwa yanagusa moja kwa moja ustawi wa watumishi, usimamizi wa rasilimaliwatu, uwajibikaji wa mwajiri na utekelezaji wa haki za wafanyakazi.
Bw. Mkomi alisisitiza kuwa Taasisi zote za Umma ambazo kwa mujibu wa taratibu ni waajiri, zina wajibu wa kuhakikisha zinatekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria na taratibu zinazohusu fidia kwa wafanyakazi.
Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) ni chombo kinachohakikisha wafanyakazi wanaopata madhara mathalani ajali au ugonjwa uliosababishwa na kazi wanapata fidia na huduma stahiki kwa mujibu wa sheria. Vilevile mfuko unaweka ulinzi wa mfanyakazi na wategemezi wake, uzuiaji wa ajali na magonjwa yatokanayo na kazi, pamoja na wajibu wa mwajiri katika kumlinda mfanyakazi.

Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Juma Mkomi akisaini kitabu cha wageni mara baada ya kuwasili katika Ofisi ya Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) kufungua mafunzo kwa Maafisa Rasilimaliwatu na Wahasibu kuhusu taratibu za kuwasilisha na kushughulikia madai ya fidia kwa wafanyakazi Jijini Dodoma.

Maafisa Rasilimaliwatu na Wahasibu wa Wizara na Taasisi za Umma zilizopo Dodoma wakimsikiliza Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Juma Mkomi (hayupo pichani) wakati akifungua Mafunzo kuhusu taratibu za kuwasilisha na kushughulikia madai ya fidia kwa wafanyakazi katika ukumbi wa LAPF Jijini Dodoma

Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Juma Mkomi (kushoto) akisalimiana na Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Dkt. John Mduma mara baada ya Katibu Mkuu huyo kuwasili katika Ofisi ya Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) kufungua mafunzo kwa Maafisa Rasilimaliwatu na Wahasibu kuhusu taratibu za kuwasilisha na kushughulikia madai ya fidia kwa wafanyakazi Jijini Dodoma.

Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Juma Mkomi (kushoto) akifurahia jambo mara baada ya kufungua mafunzo kwa Maafisa Rasilimaliwatu na Wahasibu kuhusu taratibu za kuwasilisha na kushughulikia madai ya fidia kwa wafanyakazi Jijini Dodoma.

