Na Veronica Mwafisi-Tanga
Tarehe 06 Oktoba, 2026
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete amekutana na Watumishi wa Umma wa Mkoa wa Tanga na kusikiliza changamoto wanazokutana nazo kwa lengo la kuzitafutia ufumbuzi kwa ustawi wa Utumishi wa Umma na maendeleo ya taifa.

Akizungumza na watumishi hao leo tarehe 06 Oktoba, 2026, Waziri Kikwete amesema kusikiliza kero na changamoto za Watumishi ni mojawapo ya jukumu lake akiwa ndiye Waziri mwenye dhamana ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.
Akizungumza katika kikao hicho, Mhe. Kikwete alitoa fursa kwa watumishi hao kuwasilisha changamoto zinazokwamisha utekelezaji wa majukumu yao na alizifanyia kazi na zilizohitaji vielelezo aliwaelekeza watendaji wa Mkoa huo kuzitafutia ufumbuzi haraka iwezekanavyo.
“Nimesikiliza changamoto zenu, zitaenda kufanyiwa kazi, tumpe muda Mkurugenzi huyu ni mgeni, ninaamini atazifanyia kazi kikamilifu,” Mhe. Kikwete ameongeza.
Waziri Kikwete ametoa wito kwa Waajiri wote kushughulikia changamoto zote za watumishi wanaowasimamia kwa wakati ikiwemo madai ya kupandishwa vyeo, madai ya uhamisho, na malimbikizo ya mishahara pamoja na madai mengine ya kiutumishi.
Aidha, kuhusu malimbikizo ya mishahara amesema Waajiri wanapaswa kuyahakiki madai hayo pamoja na kuweka viambatisho vyote muhimu vinavyohusiana na madai hayo kabla ya kuwasilisha Utumishi ili yahakikiwe na kuwasilishwa Hazina kwa ajili ya taratibu za malipo.
“Mtumishi anapaswa kupata majibu ya changamoto alizonazo kwa wakati na kama lipo nje ya mamlaka ya mwajiri liwasilishwe katika Mamlaka inayofuata ili mtumishi apewe majibu.” Ameongeza
Amesema azma ya Mhe. Rais ya kuuboresha Utumishi wa Umma na Utawala Bora ilijidhihirisha rasmi wakati akilihutubia Bunge la 13 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 14 Novemba, 2025, Mhe.Rais alisisitiza kuwa Serikali anayoingoza itaendeleza jitihada za kuimarisha maadili, nidhamu uzalendo, uwajibikaji pamoja na kusimamia haki na stahiki za Watumishi wa Umma na Watendaji mbalimbali serikalini ili kuongeza moyo wa kufanya kazi kwa bidii na uwajibikaji.

