Waziri wa Ujenzi, Mhe. Masanja Kadogosa, amekutana na kufanya mazungumzo na Mameneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) wa mikoa ya Arusha, Manyara, Kilimanjaro na Tanga, ambapo amepokea taarifa za utekelezaji wa miradi mbalimbali ya barabara pamoja na mikakati ya kukabiliana na athari zinazoweza kusababishwa na mvua za El Nino zinazotarajiwa kunyesha nchini.

Kikao hicho kimefanyika leo, Oktoba 7, 2026, jijini Arusha, ambapo Waziri Kadogosa amewataka Mameneja hao kuendelea kuchukua hatua za tahadhari, hususan katika maeneo yanayotambuliwa kuwa korofi, kwa kuhakikisha mitaro, mifereji na madaraja vinasafishwa na kufanyiwa maboresho ili kuruhusu maji ya mvua kupita kwa urahisi.

Aidha, Waziri Kadogosa amewaelekeza Mameneja hao kuhakikisha barabara zitakazoharibika kutokana na mvua zinafanyiwa matengenezo kwa wakati, ili kuendelea kuwezesha usafiri na usafirishaji kufanyika kwa ufanisi na kuhakikisha shughuli za kiuchumi na kijamii zinaendelea bila vikwazo.