NA DENIS MLOWE, KILOLO

EXIM Bank imekuwa mdhamini mkuu wa Kitonga Marathon inayotarajiwa kufanyika Oktoba 31, 2026 katika Wilaya ya Kilolo mkoani Iringa, huku ikielezwa kuwa mbio hizo zitatumika kama jukwaa la kutangaza fursa za uwekezaji, utalii, uhifadhi wa mazingira na biashara zilizopo wilayani humo.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari kuhusu maandalizi na udhamini wa mbio hizo, Meneja wa Exim Bank Tawi la Iringa, Asia Selem, alisema benki hiyo imeamua kuwa mdhamini mkuu wa Kitonga Marathon kutokana na umuhimu wa tukio hilo katika kuunganisha jamii, michezo, mazingira, utalii na maendeleo ya kiuchumi.

Selem alisema Exim Bank itaendelea kushirikiana na jamii kupitia matukio yenye kuleta pamoja wadau mbalimbali, huku Kitonga Marathon ikiwa ni moja ya fursa ya kuhamasisha wananchi kuhusu huduma za kifedha, elimu ya fedha na fursa za biashara.

Alisema wakati wa tukio hilo, Exim Bank itaendelea kutoa huduma zake za kibenki, ikiwemo huduma za ATM, mawakala, WhatsApp Banking, mikopo na huduma nyingine za kidijitali.

Aidha, alisema kupitia udhamini huo, benki hiyo inalenga kuwa karibu zaidi na jamii na kuwasaidia wananchi kuelewa namna wanavyoweza kutumia huduma za kifedha katika kukuza shughuli zao za kiuchumi na biashara.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo, Siwema H. Jumaa, alisema lengo la Kitonga Marathon ni kuhamasisha utunzaji wa mazingira na uhifadhi wa maliasili za Mlima Kitonga, kutangaza fursa za uwekezaji na kukuza utalii wa asili pamoja na utalii wa michezo.

Alisema mbio hizo zitahusisha mbio za barabarani za kilomita tano, 10 na 21, pamoja na trail run ya Mlima Kitonga, ambayo itafungua fursa kwa wananchi na wageni kushiriki shughuli za hiking na utalii wa asili katika eneo hilo.

Mkurugenzi Siwema alisema waandaaji wanatarajia kupata washiriki wasiopungua 800, huku usajili ukiendelea.

Alisema washiriki wa mbio za kilomita tano, 10 na 21 watalipia Sh50,000, huku watakaoshiriki mbio za kupanda Mlima Kitonga wakilipa Sh70,000 na kupata T-shirt, begi, medali na namba ya mshiriki.

Katika mbio za kilomita 21, mshindi wa kwanza atapata Sh1 milioni, wa pili Sh600,000 na wa tatu Sh400,000 kwa upande wa kilomita 10, washindi watatu wa kwanza kwa wanawake na wanaume watapata Sh500,000, Sh300,000 na Sh200,000 mtawalia.