Na mwandishi Maalum, Dar es Salaam

Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tabora – Kitete zimeingia makubaliano kuanzisha huduma za uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo katika hospitali hiyo hatua inayolenga kusogeza huduma za kibingwa karibu na wananchi wa Tabora na mikoa jirani.

Akizungumza wakati wa makubaliano hayo Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge alisema mpango wa ushirikiano kati JKCI na Kitete unakuja baada ya wataalamu wa Hospitali ya Kitete kufanya ziara ya mafunzo JKCI na kujadili kuhusu namna ambavyo wanaweza kushirikiana kufikisha huduma za bingwa moyo mkoani Tabora.

Dkt. Kisenge alisema katika hatua za awali JKCI itawajengea uwezo wataalamu wa afya wa Kitete kupitia mafunzo maalum huku ikishirikiana na hospitali hiyo kuboresha mazingira ya kutolea huduma za moyo kama ilivyo kwenye matawi mengine ya JKCI.

“Kama Taasisi tunataka kusogeza huduma za kibingwa za matibabu ya moyo karibu na wananchi. Tutawajengeeni uwezo na kuboresha mazingira ya huduma ili wananchi wapate huduma bora bila kulazimika kusafiri umbali mrefu kufata huduma hizo hapa JKCI”, alisema Dkt. Kisenge.

Aidha Dkt. Kisenge alisema JKCI itawekeza katika huduma kwa wateja ili kuhakikisha wananchi wa Tabora na mikoa ya jirani ikiwemo Mwanza, Shinyanga na Singida wanapata huduma bora za uchunguzi na matibabu ya moyo.

Kwa upande wake Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tabora – Kitete Dkt. Joachim Eyembe aliushukuru uongozi wa JKCI kwa kukubali kushirikiana nao na kuahidi kuendeleza ushirikiano huo katika kuhakikisha kuwa wananchi wanapata huduma za matibabu ya moyo kwa urahisi.

“Naomba nikuhakikishie kuwa tutashirikiana kwa karibu na Taasisi hii kuhakikisha huduma bingwa za matibabu ya moyo zinapatikana mkoani Tabora kwa wakati kupitia Hospitali yetu ya Kitete ili kusaidia kuokoa maisha ya watanzania”, alisema Dkt. Eyembe.

Naye Afisa uhakiki na udhibiti Ubora kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Adelphina Ncheye alisema pamoja na makubaliano hayo wataalam hao pia wamefanya ziara katika maeneo mbali mbali ya taasisi hiyo, hivyo kupata fursa ya kujifunza mifumo ya JKCI katika utoaji wa huduma kwa wagonjwa hususan huduma kwa mteja na ubora wa huduma.

Ushirikiano kati ya JKCI na Hospitali ya Kitete unatarajiwa kuongeza upatikanaji wa huduma za moyo kwa wananchi wa Tabora na mikoa ya jirani, huku ukiimarisha uwezo wa wataalamu wa afya kutoa huduma bora na za kisasa.