NA DENIS MLOWE, KILOLO 

WILAYA ya Kilolo mkoani Iringa imeeleza kuwa Kitonga Marathon inayotarajiwa kufanyika Oktoba 31, 2026, itatumika kama jukwaa la kutangaza fursa za uwekezaji, utalii na uhifadhi wa mazingira zilizopo katika wilaya hiyo.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari kuhusu maandalizi na udhamini wa mbio hizo, Mkuu wa Wilaya ya Kilolo, Fredy Makibete, alisema tukio hilo ni muhimu katika kuitangaza Kilolo na kuwavutia watu kutoka maeneo mbalimbali nchini kutembelea na kuwekeza katika wilaya hiyo.

Makibete alisema Kilolo ina fursa nyingi za kiuchumi katika sekta za kilimo, misitu, madini na utalii, hivyo Kitonga Marathon ni sehemu ya juhudi za kuonesha fursa hizo kwa wananchi, wawekezaji na wadau kutoka ndani na nje ya Tanzania.

“Tumekuja Kilolo kufanya kazi na kuwatumikia wananchi, kuwasikiliza na kutatua kero zao kwa kushirikiana na viongozi wenzetu. Pia tunataka kuitangaza Kilolo ili watu waone fursa zilizopo katika wilaya yetu,” alisema Makibete.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo, Siwema H. Jumaa, alisema lengo la Kitonga Marathon ni kuhamasisha utunzaji wa mazingira na uhifadhi wa maliasili za Mlima Kitonga, kutangaza fursa za uwekezaji na kukuza utalii wa asili pamoja na utalii wa michezo.

Alisema mbio hizo zitahusisha mbio za barabarani za kilomita tano, 10 na 21, pamoja na trail run ya Mlima Kitonga, ambayo pia itafungua fursa kwa wananchi na wageni kushiriki shughuli za hiking na utalii wa asili katika eneo hilo.

Mkurugenzi Siwema H Jumaa amesema kuwa wanatarajia kupata washiriki wasiopungua 800, huku usajili ukiendelea. Washiriki wa mbio za kilomita tano, 10 na 21 watalipia Sh50,000, huku watakaoshiriki mbio za kupanda Mlima Kitonga wakilipa Sh70,000 na kupata T-shirt, begi, medali na namba ya mshiriki.

Katika mbio za kilomita 21, mshindi wa kwanza atapata Sh1 milioni, wa pili Sh 600,000 na wa tatu Sh 400,000, huku katika kilomita 10 washindi watatu wa kwanza wakipata Sh500,000, Sh300,000 na Sh200,000 mtawalia kwa upande wa wanawake na wanaume.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo, Rashid Nzelemera, alisema marathon hiyo ni fursa ya kiuchumi na kijamii kwa wilaya hiyo, akisema Mlima Kitonga unaweza kuwa chanzo cha fursa mbalimbali ikiwemo uwekezaji katika hoteli na huduma nyingine za utalii.

Naye Meneja wa Exim Bank Tawi la Iringa, Asia Selem, ambao ndio wadhamini wakuu wa Kitonga Marathon alisema benki hiyo imeamua kuwa mdhamini mkuu wa Kitonga Marathon kwa kutambua umuhimu wa tukio hilo katika kuunganisha jamii, michezo, mazingira, utalii na maendeleo ya kiuchumi.

Selem alisema Exim Bank itaendelea kutoa huduma zake za kibenki wakati wa tukio hilo, huku akiwataka wananchi kutumia huduma za benki hiyo ikiwemo ATM, mawakala, WhatsApp Banking, mikopo na huduma nyingine za kidijitali. 

Alisema kupitia Kitonga Marathon, benki hiyo pia inalenga kushirikiana na jamii katika kuhamasisha elimu ya fedha na fursa za biashara.

Waandaaji wamewahimiza wananchi kutoka maeneo mbalimbali nchini kujitokeza kushiriki Kitonga Marathon, wakisema tukio hilo litakuwa sehemu ya kuitangaza Kilolo, kuvutia wawekezaji na kuonesha fursa za utalii, mazingira na biashara zilizopo katika wilaya hiyo.