Bodi za Wakurugenzi katika mamlaka za maji zinatakiwa kutosubiri taarifa bali kuhoji, kuełek eza na kusimamia kuhakikisha matokeo kwa kazi zilizopangwa.
Naibu Waziri wa Maji Mhe. Mhandisi Kundo Andrew Mathew (Mb)amesema bodi yenye malengo inakuwa na vipaumbele vinavyo pimika na kutoa suluhu ya changamoto za sasa na zijazo.
Amesema hayo akizindua bodi ya tisa ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Moshi (MUWSA) na kueleza kipimo cha kwanza cha utendaji kwa bodi ni suala la kudhibiti upotevu wa maji (NRW).
“Nawapongeza sana wajumbe walioteuliwa kuiongoza bodi hii ya tisa, uteuzi huu si heshima pekee bali ni dhamana ya kusimamia rasilimali za wananchi na kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma bora salama na endelevu” Mhe. Kundo amesema.
Ameeleza maeneo mahususi ya kufanyiwa kazi ni pamoja na ulinzi wa vyanzo vya maji, matumizi ya teknologia ya kubaini mivujo na uchambuzi wa matumizi ya maji.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji Bi Rose Ambrose ameielekeza Menejimenti na Watumishi wa MUWSA kuipa ushirikiano wa kutosha bodi ya tisa kama ambavyo wamekuwa wakifanya wakati wote kwa bodi zilizopita ili iweze kutimiza majukumu ipasavyo.
Naye Mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi ya MUWSA iliyoteuliwa Prof. Alfred Sife amesema bodi hiyo inaenda kufanyia kazi maelekezo yote yaliyotolewa katika hafla hiyo.

