Afisa Mkuu wa Udhibiti wa Yas Tanzania, Bi. Sylvia Balwire (katikati), akishirikiana na viongozi waandamizi wa Yas na Mixx kukata keki kuashiria uzinduzi wa Wiki ya Huduma kwa Wateja wakati wa hafla iliyofanyika Rock City Mall jijini Mwanza jana. Kupitia uzinduzi huo, wiki hii, timu za Yas na Mixx zitawafikia wateja masokoni kote nchini kutatua changamoto zao, huku wateja watakaotembelea maduka ya Yas na Mixx watapata fursa ya kujishindia zawadi mbalimbali.

……………… 

Mwanza, Oktoba 5, 2026 – Wateja wa Yas na Mixx wataweza kupata msaada wa huduma moja kwa moja masokoni kote nchini, huku wakijishindia zawadi katika maduka ya kampuni hizo, kupitia Wiki ya Huduma kwa Wateja iliyozinduliwa leo jijini Mwanza na itakayoendelea hadi Oktoba 9.

Uzinduzi huo umefanyika Rock City Mall,jijini Mwanza ambapo viongozi mbalimbali wa chapa hizo wamesema kaulimbiu ya mwaka huu, ‘The Extra Mile’, inasisitiza wajibu wa kwenda hatua ya ziada katika kumhudumia mteja, ikiwemo kumsikiliza, kumpa msaada kwa wakati na kutimiza ahadi anazopewa.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi wa Huduma kwa Wateja wa Yas, Mwangaza Matotola, amesema timu za Yas na Mixx zitafika katika masoko makubwa nchini kukutana na wateja, kusikiliza maoni yao na kutatua changamoto zao papo hapo. Jijini Mwanza, timu hizo zitakuwa katika soko kuu la Mwanza.

Matotola ameahidi kuwa maoni na mrejesho wote wa wateja utafanyiwa kazi, na wateja watapewa taarifa za hatua zilizochukuliwa kupitia njia mbalimbali za mawasiliano za kampuni. Changamoto zinazohitaji uchunguzi zaidi zitafuatiliwa hadi zipatiwe ufumbuzi.

“Tunapomsaidia mteja kupata suluhisho kwa wakati, maana yake tunawezesha mambo yake biashara yake, urahisi wa mawasiliano na familia yake au kukamilisha jambo lililokuwa limekwama,” amesema Matotola.

Bi Matotola pia amewashukuru wateja wa Yas zaidi ya milioni 33 kwa kuendelea kuwaamini na kuwachagua kila siku, akisema imani hiyo inaongeza wajibu wa kuhakikisha wanapata huduma bora kila siku. 

Ameongeza kuwa Huduma bora kwa wateja ni pamoja na kuhakikisha wanatoa Huduma za viwango na ndio maana Yas imewekeza zaidi ya Sh trilioni 1.2 katika kupanua na kuboresha mtandao wake wenye minara zaidi ya 4,900, ili kuwawezesha wateja kupata mawasiliano ya uhakika kwa ajili ya biashara, elimu na shughuli za kila siku.

Katika wiki hii, maduka ya Yas na Mixx yatakuwa na shughuli za kusherehekea pamoja na wateja, ambapo wateja watajishindia zawadi mbalimbali kupitia michezo shirikishi kama kuzungusha gurudumu (spin the wheel) na kujibu maswali. Kila mteja atakayefika dukani atapata zawadi na keki.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Mixx, Arnold Ngarashi, amesema kwa kutambua umuhimu wa uhakika, uthabiti na msaada wa haraka kwenye miamala ya simu wanahakikisha wanaenda extra mile katika kuwahudumia wateja wao. 

“Tunapopokea changamoto ya mteja, tunaishughulikia kwa kuelewa umuhimu wa fedha hizo kwake.

Kuwatambua watoa huduma

Wiki hii pia itatumika kuwasherehekea watoa huduma wa Yas na Mixx wanaofanya kazi nyuma ya pazia, sambamba na wale wanatoa huduma katika maduka mbalimbali ya Yas na Mixx yaliyoenea nchi nzima.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Afisa Mkuu wa Masuala ya Udhibiti – Yas Tanzania, Sylvia Balwire, alisisitiza dhamira ya kampuni hiyo ni kuendelea kutoa huduma zilizojengwa juu ya misingi ya uaminifu, uwazi na ulinzi madhubuti wa taarifa za wateja.

“Kaulimbiu ya “The Extra Mile” inaakisi kujitolea kwa Yas na Mixx katika kulinda taarifa za wateja, kutoa mawasiliano yaliyo wazi na ya kuaminika, pamoja na kuendelea kuboresha uzoefu wa wateja kupitia maoni yao na utoaji wa huduma kwa uwajibikaji” alisema.

Wateja wanahimizwa kushiriki katika shughuli za wiki hii na kutoa maoni yao. Wanaweza kupata msaada kwa kupiga namba 100, kutembelea maduka zaidi ya 567 nchini, au kuwasiliana kupitia @yastanzania_ na @mixx.tz.