Mkurugenzi wa shule za Ghati Memorials na Nyahiri Tanzania ,Michael Kembaki akizungumza katika mahafali hayo jijini Arusha .
……………..
Happy Lazaro, Arusha.
ARUSHA: WAHITIMU nchini wametakiwa kutokomea katika kutafuta vyeti, bali kujikita katika kupata maarifa yatakayowawezesha kutatua changamoto za maisha na kutimiza ndoto zao.
Hayo yamesemwa jijini Arusha na Mkurugenzi wa shule za Ghati Memorials na Nyahiri Tanzania ,Michael Kembaki wakati akizungumza katika mahafali ya 13 ya darasa la saba ambapo jumla ya wanafunzi 141 wamehitimu katika shule hiyo ya Ghati Memorial iliyopo mjini hapa.
Kembaki amesema licha ya kauli iliyozoeleka kwamba elimu ni ufunguo wa maisha, kwake maarifa ndiyo ufunguo wa maisha kwa sababu mtu mwenye maarifa hutambua uwezo wake, anajua anachokitaka na huweza kutumia alichojifunza kukabiliana na changamoto zinazomzunguka.
Kembaki amesema wahitimu wanapoendelea na elimu ya sekondari na baadaye chuo kikuu, wanapaswa kuhakikisha kila wanachosoma kinawaongezea maarifa na uwezo wa kutatua changamoto zao binafsi, familia, jamii na taifa, badala ya kusubiri kupata cheti pekee.
Aidha, amewataka wanafunzi kutambua ndoto zao na kuzilinda kwa kujituma, akisema kutimiza ndoto si jambo rahisi kwa kuwa safari hiyo inaweza kuambatana na changamoto mbalimbali, hivyo hawapaswi kukata tamaa wanapokutana na masomo magumu au vikwazo vingine.
Ametoa mfano wa mwanafunzi anayetamani kuwa daktari ambaye anaweza kukutana na ugumu katika masomo ya Biology, Chemistry na Physics, akisisitiza kuwa ugumu wa masomo hayo usiwe sababu ya kuachana na ndoto hiyo, bali mwanafunzi atafute maarifa na njia za kukabiliana na changamoto.
Kembaki pia amewataka wahitimu kusimamia ndoto zao hata pale wanapokutana na maamuzi au mipango inayoweza kuwaelekeza kwenye fani tofauti na wanazozitamani, akisisitiza umuhimu wa kuwa na msimamo, uvumilivu na kufanya kazi kwa bidii ili kufikia malengo yao.
Ameongeza kuwa, kutimiza ndoto kunahitaji pia kujinyima baadhi ya mambo, akitumia mfano wa mtu anayesafiri kwenda sokoni ambaye anapaswa kuchagua njia moja ya kufika anakoelekea, badala ya kutaka kutumia njia zote kwa wakati mmoja.
“Shule yetu imejipanga kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa kuwekeza katika miundombinu na teknolojia, ikiwemo madarasa yenye mazingira mazuri, meza na viti vya kisasa pamoja na vifaa vya kidijitali vya kufundishia.”amesema Kembaki.
Amesema shule imeanza kuwajengea uwezo walimu kutumia kompyuta na projecta katika ufundishaji, hatua inayolenga kuondoa mfumo wa zamani wa kufundisha kwa kukaririsha wanafunzi na badala yake kutumia mbinu za kisasa zinazosisitiza uelewa na vitendo.
Amefafanua kuwa, shule pia ina mpango wa kutumia teknolojia zaidi katika ujifunzaji, ambapo wanafunzi wa madarasa mbalimbali wanatarajiwa kutumia tablet zenye vitabu vya kielektroniki, huku shule ikiboresha huduma ya intaneti ili wanafunzi waweze kuitumia katika maeneo mbalimbali ya shule.
“Shule yetu imeanza kuchukua hatua za kupanua eneo la michezo kwa kununua eneo lililopo nyuma ya majengo ya shule, huku ikipanga kuondoa baadhi ya majengo na kufanya taratibu za kuondoa majengo ya jirani ili kupata eneo kubwa litakalotumika kwa michezo mbalimbali.”amesema Kembaki.
Aidha, amesema shule ina mpango wa kujenga ukumbi utakaotumika kwa mafunzo ya vitendo na kuwafundisha wanafunzi stadi za maisha (Life Skills), ili kuwajengea uwezo wa kukabiliana na changamoto za maisha na kuwaandaa kwa ushindani katika soko la ajira pamoja na kujiajiri.
Amesema pamoja na maandalizi hayo, shule inatambua changamoto ya ukosefu wa ajira na ushindani mkubwa uliopo katika dunia ya sasa, hivyo inalenga kuwajengea wanafunzi uwezo ambao hautawaandaa kutafuta ajira pekee, bali pia kuwasaidia kujiajiri na kutumia vipaji na maarifa yao kujitengenezea fursa.
Katika risala yao, wanafunzi wameishukuru shule kwa kuwapatia mazingira mazuri ya kujifunzia, ikiwemo madarasa, meza na viti vya kisasa pamoja na matumizi ya vifaa vya kidijitali kama projecta katika ufundishaji na ujifunzaji.
Wamesema pamoja na mafanikio hayo, shule bado inakabiliwa na changamoto ikiwemo ukosefu wa viwanja vya michezo na uhaba wa baadhi ya vifaa vya kujifunzia, hususani kompyuta na projekta, hali wanayoamini inaweza kuathiri fursa za wanafunzi kuendeleza vipaji vyao.
Wanafunzi wameiomba shule na wadau wengine kuendelea kusaidia upatikanaji wa viwanja vya michezo, kujenga maktaba ya kisasa, kuongeza kompyuta na kuhamasisha wazazi kulipa ada kwa wakati ili kuhakikisha wanafunzi wanapata mazingira bora ya kujifunza na kuendeleza vipaji vyao.

