Katibu Tawala Mkoa wa Rukwa Msalika Robert Makungu akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa Mkuu wa mkoa kwa niaba ya Katibu Mkuu -Ofisi ya Rais maendeleo ya vijana Jenifa Omolo.
………………
Na Neema Mtuka, Sumbawanga
RUKWA: Mkoa wa Rukwa umetangaza kukamilisha kwa kiwango kikubwa maandalizi ya maadhimisho ya Wiki ya Vijana Kitaifa yatakayofanyika mkoani humo kuanzia Oktoba 8 hadi 14, 2026.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Oktoba 5, 2026, kwa niaba ya Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana, Jenifa Omolo, katika ukumbi wa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Katibu Tawala wa Mkoa huo, Msalika Robert Makungu, amesema maadhimisho hayo yatafanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Ndua, Manispaa ya Sumbawanga.
Makungu amesema Wiki ya Vijana mwaka huu itaenda sambamba na matukio mawili makubwa ya kitaifa, ambayo ni kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru na Maadhimisho ya Miaka 27 ya Kifo cha Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, yatakayofanyika Oktoba 14 katika Uwanja wa Nelson Mandela.
“Kwa mujibu wa ratiba, kuanzia Oktoba 8 hadi 14, viwanja vya Ndua vitakuwa kitovu cha shughuli za vijana kutoka kila mkoa wa Tanzania Bara na Zanzibar,” amesema Makungu.
Amesema kutakuwa na maonesho ya ubunifu wa vijana, bidhaa za wajasiriamali, taasisi za serikali, sekta binafsi, fursa za mikopo pamoja na majadiliano kuhusu sera za vijana.
Ameongeza kuwa vijana 1,500 wanatarajiwa kushiriki katika maadhimisho hayo kwa kuonesha vipaji vya sanaa na utamaduni vyenye ujumbe wa umoja wa kitaifa, kujitegemea, kufanya kazi kwa bidii, uzalendo na kuwajibika kwa jamii.
Katibu Tawala huyo amewataka wananchi wa Rukwa na wafanyabiashara kuchangamkia fursa za kiuchumi zitakazotokana na ujio wa wageni kutoka ndani na nje ya nchi, ikiwemo Zanzibar.
Maadhimisho hayo yanaratibiwa na Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa.
Aidha, ufunguzi rasmi wa Wiki ya Vijana Kitaifa utafanyika Oktoba 10, 2026, katika viwanja vya Shule ya Msingi Ndua, Kata ya Kizwite, Manispaa ya Sumbawanga, ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba.
Makungu amesema Serikali inatarajia kuona vijana wengi zaidi wakipata taarifa kuhusu fursa zinazopatikana serikalini na kwa wadau wengine, kupata huduma, kujenga mitandao na kuonesha shughuli wanazofanya.
Amesema timu ya kitaifa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu na Zanzibar tayari imekagua viwanja hivyo na kuridhishwa na maandalizi.
