Na.Sophia Kingimali.
WAZIRI wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar, amezitaka nchi na taasisi za kimataifa kubadili mfumo wa utoaji wa fedha za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, akisisitiza kuwa nchi zinazoendelea hazipaswi kulazimika kuongeza mzigo wa madeni ili kukabiliana na changamoto ambayo imeathiri dunia kwa ujumla.
Hayo ameyasema leo Octoba 5,2026 Jijini Dar es salaam wakati akifungua mkutano wa majadiliano kuhusu upatikanaji wa fedha za ufadhiri kukabiliana na mabadiliko ya Tabia Nchi kwa mwaka 2026 amesema Tanzania inahitaji dola bilioni 19.3 za Marekani kutekeleza mahitaji yake ya kukabiliana na mabadiliko hayo, lakini upatikanaji wa fedha hizo bado ni changamoto kutokana na kiwango kidogo cha rasilimali kinachotengwa kwa nchi zinazoendelea.
Balozi Khamis amesema sehemu kubwa ya fedha zinazotolewa kwa ajili ya miradi ya tabianchi huja kwa mfumo wa mikopo, hali ambayo inaweza kuongeza mzigo wa madeni kwa nchi ambazo tayari zinahitaji rasilimali kubwa kwa ajili ya maendeleo.
Amesema Tanzania inapendekeza kuongezwa kwa fedha zenye masharti nafuu, ruzuku na rasilimali za ziada zinazoweza kutabirika, pamoja na kuharakishwa kwa mifumo ya blended finance, malipo yanayotokana na matokeo na kubadilisha madeni kuwa uwekezaji katika miradi ya tabianchi na uhifadhi wa mazingira.
Aidha ameongeza kuwa Tanzania pia inahitaji ushirikiano wa kimataifa katika kuvutia mitaji binafsi kwenye sekta za nishati jadidifu, kilimo na maeneo mengine yanayoweza kuongeza uwezo wa kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Amesema nchi hiyo inaendelea kuchukua hatua kwa kuongeza uzalishaji wa nishati jadidifu, ikiwamo nishati ya jua na jotoardhi, huku hatua hizo zikilenga kupunguza utegemezi wa nishati za mafuta, kulinda misitu na kuboresha afya za wananchi.
Balozi Khamis amesema Tanzania tayari imeanza kujenga soko la fedha endelevu, akitolea mfano dhamana ya kijani iliyotolewa mwaka 2023 na mamlaka ya maji, ambayo ilipata mwitikio mkubwa kutoka kwa wawekezaji na kuonyesha uwezekano wa kutumia masoko ya mitaji kufadhili miradi ya mazingira.
Amesema Tanzania iko tayari kushirikiana na wadau wa kimataifa katika kutafuta suluhisho la pengo la fedha za tabianchi, akisisitiza kuwa lengo kuu linapaswa kuwa kuhakikisha rasilimali zinabadilika kuwa miradi yenye matokeo halisi kwa wananchi, ajira na fursa za maendeleo.

