NA SILIVIA AMANDIUS 

KAGERA.

Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Kanali Yahya Kido, amemtaka Mkuu mpya wa Wilaya ya Misenyi, Kanali Isaac Anthony Mwakisu, kuweka mbele masuala ya ulinzi na usalama, kudhibiti uhamiaji haramu na kuhakikisha vitendo vya utoroshaji wa mazao ya biashara, ikiwemo kahawa, vinadhibitiwa kutokana na wilaya hiyo kuwa katika eneo la mpakani.

Kanali Kido ametoa maagizo hayo wakati wa hafla ya kumkaribisha Kanali Mwakisu ambaye amehamia Misenyi akitokea Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma Leo October 5, 2026 ambako amesema amehudumu kwa takribani miaka mitano na miezi kadhaa. Amesema uteuzi huo ni ishara ya imani aliyopewa na Rais na kwamba anapaswa kutumia nafasi hiyo kushirikiana na watendaji pamoja na wananchi kuhakikisha Wilaya ya Misenyi na Mkoa wa Kagera kwa ujumla vinaendelea katika nyanja za kiuchumi na kijamii.

Katika eneo la ulinzi na usalama, Kanali Kido amesisitiza umuhimu wa kuimarisha ujirani mwema na wilaya za jirani pamoja na maeneo ya mipakani. Pia amemtaka Mkuu huyo mpya kusimamia kwa karibu maandalizi ya kukabiliana na athari zinazoweza kujitokeza kutokana na mvua za El Niño, ikiwemo kutembelea maeneo hatarishi na kuwahimiza wananchi kuchukua hatua za tahadhari mapema.

Katika suala la mapato, Kanali Kido amemtaka Kanali Mwakisu kusimamia kwa karibu ukusanyaji wa mapato ya Halmashauri ya Wilaya ya Misenyi, ambayo imewekewa lengo la kukusanya shilingi bilioni 14.5. Amesisitiza umuhimu wa kuwa na ushirikiano mzuri kati ya viongozi wa wilaya, halmashauri na watendaji wanaohusika na usimamizi wa mapato ili kuhakikisha lengo hilo linafikiwa.

Mkuu huyo wa Mkoa amemtaka pia kusimamia shughuli za kilimo na uzalishaji, akieleza kuwa sekta hiyo ni muhimu katika kukuza uchumi wa wananchi. Katika elimu, amesisitiza maandalizi ya kutosha ya miundombinu na mazingira ya kujifunzia kutokana na ongezeko la wanafunzi linalotarajiwa katika miaka ijayo, akiwataka viongozi kujiandaa mapema badala ya kusubiri changamoto zijitokeze.

Kanali Kido amesisitiza pia umuhimu wa kusikiliza kero na malalamiko ya wananchi, akisema ushirikiano kati ya Serikali, chama, taasisi na wananchi ni msingi wa kujenga jamii yenye amani na maendeleo. Amewataka watumishi wa Serikali katika Wilaya ya Misenyi kumpa ushirikiano mkubwa Mkuu huyo mpya ili aweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.

Kwa upande wake, Kanali Isaac Anthony Mwakisu amemshukuru Mkuu wa Mkoa pamoja na viongozi wa Wilaya ya Misenyi kwa mapokezi aliyoyapata, akiahidi kutekeleza maagizo yote yaliyotolewa na Mkuu wa Mkoa.

Kanali Mwakisu amesema ulinzi na usalama ni jukumu la kila mmoja, hivyo atafanya kazi kwa kushirikiana na watendaji wa Serikali pamoja na wananchi kuhakikisha amani na usalama vinaendelea kuimarika katika wilaya hiyo.

Amesema pia atahakikisha fedha zinazotolewa na Serikali kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo zinasimamiwa kwa umakini na kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa ili wananchi wanufaike na uwekezaji unaofanywa na Serikali.

Aidha, Mkuu huyo mpya wa Wilaya ya Misenyi ameahidi kuwa utawala wake utazingatia usikivu kwa wananchi, akieleza kuwa atatenga muda maalumu wa kusikiliza kero zao na kushirikiana na watendaji kuzitafutia ufumbuzi.

Hafla ya mapokezi imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo wakuu wa idara na vitengo, viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Misenyi pamoja na wadau wengine. Baada ya hafla hiyo, Kanali Isaac Anthony Mwakisu anakabidhiwa rasmi ofisi na aliyekuwa Mkuu wa Wilaya hiyo, ambaye amemaliza muda wake baada ya kuhudumu Misenyi kwa zaidi ya miaka miwili.