Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Manyara Regina Qwaray kikabidhi vitimwendo saba kwa watoto wenye mahitaji maalum, hususan wenye ulemavu wa viungo, ikiwa ni hatua inayolenga kurahisisha maisha yao ya kila siku ili waweze kushiriki kikamilifu katika shughuli za kijamii na kielimu.
………….
Na Mwandishi Wetu, Simanjiro
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Regina Qwaray, ametoa vitimwendo saba kwa watoto wenye mahitaji maalum, hususan wenye ulemavu wa viungo, ikiwa ni hatua inayolenga kurahisisha maisha yao ya kila siku.
Mhe. Qwaray, ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Manyara, amesema ameamua kutoa msaada huo kwa kuzingatia umuhimu wa jamii kuwasaidia watoto wenye mahitaji maalum ili waweze kushiriki kikamilifu katika shughuli za kijamii na kielimu.
Akikabidhi vitimwendo hivyo leo wilayani Simanjiro, Mhe. Qwaray amesema kila anapopata nafasi na uwezo wa kusaidia, huwakumbuka watoto wenye mahitaji maalum kwa kuwa wanahitaji msaada na uangalizi zaidi kutoka kwa jamii.
Amesema hatua hiyo pia ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kusaidia na kutetea haki za makundi yenye mahitaji maalum katika jamii.
Mhe. Qwaray amesema vitimwendo hivyo vitasaidia kupunguza mzigo kwa wazazi na walezi ambao hulazimika kuwabeba watoto wenye ulemavu wanapokwenda shule au kushiriki shughuli nyingine za kijamii.
Amewataka watoto walionufaika na msaada huo kuvithamini na kuvitunza ili viweze kuwasaidia kwa muda mrefu.
Aidha, ameitaka jamii kutowaficha watoto wenye mahitaji maalum, bali kuwapa nafasi ya kupata elimu na kushiriki katika shughuli mbalimbali kama ilivyo kwa watoto wengine.
Mhe. Qwaray pia ametoa wito kwa watu wenye uwezo kujitokeza na kuwasaidia watoto na watu wengine wenye mahitaji maalum kwa kuwapatia mahitaji mbalimbali kulingana na uwezo wao.
Kwa upande wao, wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) wa Halmashauri ya Simanjiro ambao ni madiwani, wamempongeza Qwaray kwa kujitoa kuwasaidia watoto hao na kuwataka viongozi pamoja na wadau wengine kuiga mfano huo.
Baadhi ya wazazi walionufaika na msaada huo wamemshukuru Mhe.Qwaray, wakisema vitimwendo hivyo vitawasaidia kurahisisha maisha ya watoto wao na kuwawezesha kushiriki katika shughuli mbalimbali.
Wamesema msaada huo utapunguza changamoto ya kuwabeba watoto wao mgongoni, hasa wanapokwenda shule au kushiriki shughuli nyingine za kijamii.

