Na Mwandishi wetu, Mirerani 

CRDB Bank Tawi la Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, imeadhimisha wiki ya huduma kwa wateja kwa wadau wa benki hiyo na wafanyakazi wa benki hiyo kukutana na kujadili masuala mbalimbali ikiwemo fursa zilizopo.

Meneja wa CRDB Tawi la Mirerani, Renatus Rutajama akizungumza kwenye tafrija na wateja hao iliyofanyika ukumbi wa Tanzanite Palace Hotel, amesema kauli mbiu ya mwaka huu ni ‘The Extra mile.’ 

Rutajama amewashukuru wateja wao waliokutana kwa pamoja ambao wametenga muda wao ili kuadhimisha wiki ya huduma kwa wateja.

‘Leo ni siku ya uzinduzi wa wiki ya huduma kwa wateja kuanzia Oktoba 5 kwa muda wa wiki nzima tunaadhimisha wiki ya huduma kwa wateja,” amesema Rutajama.

Amesema kama mteja amekuja kwenye benki na kufuata huduma moja ya kufungua akaunti anapaswa kuongezewa na huduma nyingine ili kukamilisha dhima ya mwaka huu ya The Extra Mile.

Amesema wamepokea maoni yote ikiwemo kuboresha huduma maeneo mengine ya wilaya ya Simanjiro ikiwemo Terrat, Naberera na sehemu ambazo hawana matawi.

“Tumepokea maelezo yao kwani CRDB ina matawi mengi hadi nje ya nchi ikiwemo Burundi, Congo, Dubai na China, hivyo hayo maeneo wanayotaja kwa hapa Simanjiro tutafika kufungua matawi na mawakala,” amesema.

Afisa mwingine wa benki hiyo Adam Mgaza amewaasa wafanyabiashara wa eneo hilo kuwa na utamaduni wa kukutana na kujadiliana na baadhi ya wateja wao na kama CRDB Tawi la Mirerani walivyofanya.

“Mpendwa mteja, Benki ya CRDB inakutakia Heri ya Wiki ya Huduma kwa Wateja! Ni fahari yetu kukuhudumia na kuendelea kukupatia huduma bora kila wakati,” amesema Mgaza.

Paroko wa Parokia ya Bikira Maria Malkia wa Rozali Takatifu Mji mdogo wa Mirerani, Padri Aristarki Tarimo amewapongeza CRDB kwa kuwakutanisha wateja wao na watumishi wa benki hiyo katika wiki ya huduma kwa wateja.

Sheikhe wa Wilaya ya Simanjiro, Ramia Ramadhani amesema CRDB inatoa huduma bora hivyo ifungue matawi maeneno mengine ya Simanjiro ikiwemo Terrat na Naberera.

Mmoja wa mawakala wa CRDB mji mdogo wa Mirerani, Abraham Macha ameeleza kuwa umoja, mshikamano na upendo baina ya benki na wateja inatakiwa iwepo kwenye huduma ili kuachiana tabasamu.