Spika wa Bunge la Wawakilishi la Uingereza (House of Commons), Sir Lindsay Hoyle, amewasili jijini Arusha usiku wa tarehe 3 Oktoba 2026 kwa ajili ya kushiriki Mkutano wa 153 wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), unaotarajiwa kufanyika kuanzia tarehe 5 hadi 9 Oktoba 2026 katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC).

Sir Lindsay Hoyle ni miongoni mwa viongozi wa mabunge kutoka nchi wanachama wa IPU wanaoendelea kuwasili nchini Tanzania kwa ajili ya kushiriki mkutano huo wa kimataifa unaowakutanisha Maspika wa Mabunge, wabunge, maafisa wa mabunge pamoja na wawakilishi wa taasisi mbalimbali za kimataifa.

Viongozi wengine waliowasili usiku wa tarehe 3 Oktoba 2026 kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) ni pamoja na Maspika na Naibu Maspika kutoka India, Angola, Malaysia na Bhutan, ambao pia watashiriki katika majadiliano mbalimbali yatakayofanyika wakati wa mkutano huo.

Mkutano wa 153 wa IPU unaofanyika Arusha, Tanzania, unatarajiwa kuwakutanisha zaidi ya wajumbe 2,000 kutoka mabunge ya nchi wanachama wa IPU pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo kutoka duniani kote.

Mkutano huo ni jukwaa muhimu la kujadili masuala ya utawala bora, demokrasia, maendeleo endelevu na namna ya kuimarisha ushirikiano wa kimataifa katika kukabiliana na changamoto zinazoikabili dunia.