Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenérali Ahmed Abbas katikati akiwa na Brigedia Jenérali John Ndunguru wa pili kulia na Katibu Tawala wa Mkoa huo Mary Makondo wa pili kushoto

………

Na Mwandishi wetu, Songea

MKUU wa Mkoa wa Ruvuma, Brigedia Jenerali Ahmed Abbas, amewataka watumishi wa umma kuwa waadilifu na waaminifu katika kutekeleza majukumu yao ya kuwahudumia wananchi, huku akiwasisitiza kumtanguliza Mungu katika kila jambo.

Akizungumza wakati wa hafla ndogo ya kumuaga Brigedia Jenerali John Ndunguru, ambaye alikuwa mjumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Ruvuma na ambaye anahamia Mkoa wa Tabora.

Mkuu wa Mkoa amesema, kila mtu amewekwa katika nafasi yake na Mungu, hivyo binadamu yeyote hawezi kubadili nafasi ya mtu mwingine. Kutokana na hali hiyo, amewataka watumishi wa umma kushirikiana badala ya kufanyiana hila zinazoweza kuharibu nafasi za wenzao.

Akiwaaga wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Ruvuma pamoja na wakuu wa taasisi mbalimbali wa mkoa huo, Brigedia Jenerali John Ndunguru ambaye anahamia Mkoa wa Tabora, amewataka viongozi kuwa watulivu na waaminifu kwa watu wanaowaongoza ili kuleta tija katika jamii.

Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma Wakili Mary Makondo, amesema,uongozi ni kujali na kugusa maisha ya jamii unayoiongoza.

Ameongeza kuwa anamshukuru Brigedia Jenerali John Ndunguru kwa kuwa kiongozi aliyejali na kugusa maisha ya jamii aliyokuwa akiiongoza.