NA DENIS MLOWE, IRINGA
MBUNGE wa Jimbo la Kalenga, Jackson Kiswaga, ametunukiwa tuzo maalumu na Shule ya Msingi Mwenge iliyopo Kata ya Nzihi, Wilaya ya Iringa, kwa kutambua mchango wake katika kuunga mkono maendeleo ya elimu, afya na miundombinu katika jamii.
Tuzo hiyo imekabidhiwa kwa Mbunge Kiswaga na mdau wa elimu, Mama Rob, katika hafla ya kumaliza darasa la saba iliyofanyika shuleni hapo, ambapo viongozi, walimu, wazazi na wananchi walipata nafasi ya kushuhudia tukio hilo.
Akizungumza kabla ya kukabidhi tuzo hiyo na Mama Rob kama mgeni mashuhuri ambapo Mbunge Kiswaga alikuwa mgeni rasmi Mwalimu Mkuu shule ya msingi Mwenge Fredrick Chota
amesema utambuzi huo umetokana na mchango na ushirikiano ambao Mbunge Kiswaga amekuwa akitoa katika kusaidia maendeleo ya jamii, hususan katika maeneo yanayogusa maisha ya wananchi moja kwa moja ikiwemo sekta ya elimu hususan katika shule hiyo.
Alisema kuwa Mbunge Kiswaga amesaidia kwa kupatikana kwa umeme shuleni hapo utoaji wa mifuko 70 ya saruji. Mabati 60 na ahadi ya ununuzi wa mashine ya kurudufu itakayoghariku sh milioni 2.5
Amesema kuwa mchango katika sekta ya elimu ni sehemu muhimu ya kujenga kizazi chenye maarifa, huku akieleza kuwa jitihada za viongozi na wadau mbalimbali zinapounganishwa, huleta matokeo chanya katika kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia.
Kwa upande wake, Mbunge Kiswaga ameshukuru uongozi wa Shule ya Msingi Mwenge pamoja na Mama Rob kwa kutambua mchango wake, akisema tuzo hiyo kwake ni ishara ya kuendelea kushirikiana na wananchi katika kutatua changamoto zinazowakabili.
Alisema kuwa tuzo hiyo, sehemu ya matokeo ya jitihada za pamoja zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye amekuwa akihakikisha fedha zinatengwa na kutolewa kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo katika maeneo mbalimbali nchini.
Kiswaga alisema kuwa katika kipindi cha uongozi wa Rais Samia, wananchi wameendelea kushuhudia utekelezaji wa miradi katika sekta muhimu zikiwemo elimu, afya, maji na miundombinu, akieleza kuwa upatikanaji wa fedha za Serikali umewezesha viongozi na wananchi kutekeleza mahitaji mbalimbali yaliyokuwa yakisubiriwa kwa muda mrefu.
Alisema mafanikio yanayoonekana katika Jimbo la Kalenga hayawezi kutenganishwa na juhudi za Serikali chini ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha fedha za miradi zinafika kwenye maeneo husika, huku akitaja ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya elimu, afya pamoja na barabara kuwa miong3oni mwa maeneo ambayo yameendelea kupata msukumo kupitia fedha za Serikali.
“Tunachofanya sisi kama viongozi ni kuwasilisha mahitaji ya wananchi, lakini utekelezaji wake unategemea Serikali kutoa fedha. Tunamshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa fedha ambazo zimewezesha miradi mbalimbali kutekelezwa na wananchi kupata huduma bora,” alisema Kiswaga.
Amesema kuwa elimu, afya na miundombinu ni maeneo muhimu katika maendeleo ya wananchi, hivyo ataendelea kushirikiana na Serikali, wadau na jamii kuhakikisha changamoto zilizopo zinapatiwa ufumbuzi kwa kadri ya uwezo na nafasi yake.
Mbunge Kiswaga amewataka wananchi kuendelea kushirikiana katika kulinda na kuboresha miundombinu ya kijamii, huku akisisitiza umuhimu wa wazazi na walezi kuhakikisha watoto wanapata elimu na mazingira bora ya kujifunzia.
Tuzo hiyo imekuwa pia sehemu ya kutambua mchango wa wadau mbalimbali wanaoshirikiana na jamii katika kuunga mkono juhudi za maendeleo, hususan katika maeneo ya elimu, afya na miundombinu.
