
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius John Ndejembi, akisalimiana na Rais wa Jamhuri ya Kiarabu ya Misri Mhe. Abdel Fattah el- Sisi wakati akiwasili katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha New Alamein nchini Misri kumwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika Mkutano wa Nane wa Kamati ya Uratibu ya Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika (8th African Union Mid-Year Coordination Summit), leo tarehe 04 Oktoba 2026.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius John Ndejembi, akiwa katika picha ya pamoja na Rais wa Jamhuri ya Kiarabu ya Misri Mhe. Abdel Fattah el- Sisi wakati akiwasili katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha New Alamein nchini Misri kumwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika Mkutano wa Nane wa Kamati ya Uratibu ya Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika (8th African Union Mid-Year Coordination Summit), leo tarehe 04 Oktoba 2026.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius John Ndejembi, akizungumza na Rais wa Senegal Mhe. Bassirou Diomaye Faye mara baada ya kuwasili katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha New Alamein nchini Misri kumwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika Mkutano wa Nane wa Kamati ya Uratibu ya Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika (8th African Union Mid-Year Coordination Summit), leo tarehe 04 Oktoba 2026.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius John Ndejembi, akiwa katika picha ya pamoja na Rais wa Senegal Mhe. Bassirou Diomaye Faye pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Afrexim Dkt. George Elombi mara baada ya kuwasili katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha New Alamein nchini Misri kumwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika Mkutano wa Nane wa Kamati ya Uratibu ya Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika (8th African Union Mid-Year Coordination Summit), leo tarehe 04 Oktoba 2026.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius John Ndejembi, akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi mbalimbali kabla ya ufunguzi wa Mkutano wa Nane wa Kamati ya Uratibu ya Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika (8th African Union Mid-Year Coordination Summit), uliofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha New Alamein nchini Misri leo tarehe 04 Oktoba 2026.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius John Ndejembi akishiriki Mkutano wa Nane wa Kamati ya Uratibu ya Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika (8th African Union Mid-Year Coordination Summit), uliofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha New Alamein nchini Misri leo tarehe 04 Oktoba 2026.
……..
NA EL ALAMEIN, MISRI
Tanzania imetaka nchi za Afrika kuongeza kasi ya kuunganisha miundombinu ya usafiri, nishati na mifumo ya kidijitali ili kurahisisha biashara, kuimarisha minyororo ya thamani na kujenga uchumi wa bara wenye uwezo mkubwa wa kukabiliana na misukosuko ya kimataifa.
Wito huo umetolewa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius John Ndejembi, wakati akihutubia Mkutano wa 8 wa Kamati ya Uratibu ya Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika uliofanyika El Alamein, Misri, Oktoba 4, 2026.
Akizungumza kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais amesema misukosuko ya kiuchumi iliyoikumba Afrika na dunia mwaka huu, kwa kiasi kikubwa imeweka changamoto katika mtangamano wa Afrika, na kuonesha umuhimu wa kuharakisha ujenzi wa viwanda, kuimarisha minyororo ya thamani ya kikanda na kuongeza biashara baina ya nchi za Afrika.
Amesema changamoto katika miundombinu, na upungufu vimejitokozea pia katika minyororo ya thamani ya bidhaa muhimu kama chakula na mbolea, hivyo kuhitaji nchi za Afrika kuchukua hatua za pamoja na za haraka. Tanzania imesema itaendelea kutekeleza wajibu wake kwa kuimarisha miundombinu ya usafiri, kuboresha huduma za usafirishaji na kurahisisha mifumo ya malipo ili kuchochea biashara.
Akieleza hatua ambazo Tanzania inachukua katika kuimarisha utengamano katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, Makamu wa Rais amesema uboreshaji wa Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA), ujenzi wa Reli ya Kisasa ya SGR inayounganisha Tanzania na Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, pamoja na uboreshaji wa bandari na miundombinu ya huduma za usafiri wa anga ni miongoni mwa jitihada zinazoendelea.
Aidha, Tanzania pia inaendelea na miradi ya kusafirisha umeme inayolenga kuunganisha East African Power Pool (EAPP) na Southern African Power Pool (SAPP), pamoja na miradi ya pamoja ya uzalishaji umeme na Burundi, Rwanda na Uganda. Kwa mujibu wa Makamu wa Rais, hatua hizo zitasaidia kuchochea utekelezaji wa Eneo Huru la Biashara la Bara la Afrika (AfCFTA), kuharakisha mtangamano na kuimarisha uwezo wa bara kustahimili misukosuko ya kiuchumi na kuvurugika kwa minyororo ya ugavi.
Pamoja na uwekezaji katika miundombinu, Makamu wa Rais amesisitiza umuhimu wa Afrika kuwa na mkakati mpana na ulioratibiwa wa matumizi sahihi ya rasilimali, akisema hatua hiyo ni muhimu katika kugharamia miradi mikubwa ya kikanda na bara yenye uwezo wa kuleta ukuaji endelevu, jumuishi na unaostahimili misukosuko.
Katika hatua inayoweka Tanzania katika mjadala mpana wa mwelekeo wa mtangamano wa Bara, Makamu wa Rais ametangaza nia ya Tanzania kupendekeza Kaulimbiu ya Mwaka 2028 ya Umoja wa Afrika kuwa “Kuunganisha Mataifa: Kuharakisha Mtangamano wa Kiuchumi wa Afrika kupitia Miundombinu.” (Bridging Borders: Accelerating African Economic Integration through Infrastructure Connectivity).
Pendekezo hilo linalenga kuweka msukumo mkubwa zaidi wa kisiasa katika miundombinu ya usafiri, nishati na kidijitali inayounganisha nchi za Afrika, sambamba na kuboresha mifumo ya biashara mipakani, kupunguza gharama za usafirishaji na kuvutia uwekezaji katika miundombinu kati ya mataifa. Pia kuunga mkono utekelezaji wa Agenda 2063 na AfCFTA, pamoja na kuimarisha viwanda na minyororo ya thamani ya kikanda.
Makamu wa Rais amefafanua kuwa Tanzania haipendekezi kuanzishwa kwa programu au taasisi nyingine mpya, bali inalenga kutoa msukumo mpya wa kisiasa na hatua za pamoja katika kutekeleza mipango ambayo Afrika tayari imejiwekea.
Amesema Bara tayari lina Sera, Mifumo na Taasisi zinazohitajika kuendeleza mtangamano, hivyo jukumu lililopo sasa ni kuongeza kasi ya utekelezaji, kuimarisha uratibu na kukusanya rasilimali zinazohitajika ili ahadi hizo zizae matokeo halisi kwa wananchi na uchumi wa Afrika.
Akisisitiza umuhimu wa ajenda hiyo, Ndejembi amesema changamoto zilizojitokeza duniani hivi karibuni zinapaswa kuipa Afrika ari mpya ya kutekeleza maono na malengo yake, akieleza kuwa kuimarika kwa mtangamano wa Bara la Afrika, kutajenga mshikamano, ustawi wa pamoja na nguvu ya kiuchumi ya mataifa ya Afrika.
Akiwasilisha Taarifa ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kwenye mkutano huo Makamu wa Rais wa Uganda, Meja (Mstaafu) Jessica Rose Epel Alupo kwa niaba ya Rais wa Uganda, Mhe. Yoweri Kaguta Museveni, amesema ustawi wa wananchi unahitaji masoko makubwa zaidi ya mipaka ya nchi moja moja, akitaja EAC, COMESA na AfCFTA kuwa muhimu kwa wakulima, wenye viwanda na wazalishaji kupata masoko ya bidhaa zao. Amesema EAC imeendelea kupunguza vikwazo vya biashara na kuimarisha mifumo ya forodha na miundombinu inayounganisha nchi wanachama.
Mkutano huo unaweka mkazo katika kuharakisha mtangamano wa Bara la Afrika na utekelezaji wa Agenda 2063, huku hoja zilizowasilishwa na viongozi zikielekeza kwenye haja ya kuunganisha masoko, miundombinu, uzalishaji na usalama ili mipango ya Afrika iweze kuleta matokeo yanayoonekana kwa wananchi.
Mkutano wa 8 wa Kamati ya Uratibu ya Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika uliofanyika El Alamein, Misri,umefunguliwa na Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika ambaye pia ni Rais wa Burundi Mhe. Évariste Ndayishimiye, na kuhududhuriwa na viongozi kutoka mataifa 15 ya Afrika, Mashirika na Taasisi za Kimataifa kujadili namna ya kuongeza kasi ya mtangamano wa Bara na utekelezaji wa vipaumbele vya maendeleo ya Afrika.
Katika Mkutano huo, Makamu wa Rais ameambatana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Idara Maalum za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mhe. Idrisa Kitwana Mustafa, Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Viwanda na Biashara Bw. Aristides Mbwasi, Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia na Mwakilishi wa kudumu Umoja wa Afrika Mhe. Innocent Shiyo pamoja na Mwenyekiti wa Bunge Mhe. Najma Murtaza Giga.
