Baadhi ya wafanyakazi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakiwa katika picha ya pamoja na tuzo ya mshindi wa tatu kwa taasisi zilizotoa huduma bora za afya wakati wa maonesho ya tisa ya kitaifa ya teknologia ya madini yaliyomalizika leo katika viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan Bombambili vilivyopo mkoani Geita.

Fundi sanifu wa moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Victoria Kazibila akiwagawia vipeperushi mwananchi wanaosubiri kupata huduma katika banda la JKCI wakati wa maonesho ya tisa ya kitaifa ya tekinologia ya madini yaliyokuwa yakifanyika katika viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan Bombambili na kumalizika leo mkoani Geita.

Baadhi ya wananchi wa mkoa wa Geita na maeneo jirani wakisubiri kupata huduma za vipimo vya moyo walipotembelea banda la Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakati wa maonesho ya tisa ya kitaifa ya teknologia ya madini yaliyokuwa yakifanyika katika viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan Bombambili na kumalizika leo mkoani Geita. (Picha na JKCI)
………..
Jumla ya watu 702 wamefanyiwa uchunguzi na matibabu ya magonjwa yasiyoambukiza yakiwemo magonjwa ya moyo wakati wa maonesho ya tisa ya kitaifa ya teknolojia ya madini.
Maonesho hayo yaliyofanyika kwa siku 10 yamemalizika leo katika viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan bombambili vilivyopo mkoani Geita ambapo idadi ya watu waliofanyiwa uchunguzi wa magonjwa ya moyo mwaka huu kuwa kubwa kuliko ya miaka ya nyuma.
Akizungumza na waandishi wa habari leo mkoani Geita daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Moses Manumbu alisema mwitikio wa wananchi kufanya uchunguzi wa afya ulikuwa mkubwa ambapo kati ya watu 702 waliopimwa watu wazima walikuwa 685 na watoto 17.
Watu wengi tumewabaini kuwa na tatizo la shinikizo la juu la damu na uzito uliopitiliza, madhara ya shinikizo la juu la damu ni makubwa jamii inapaswa kuzingatia mtindo bora wa maisha ikiwemo kufanya mazoezi na kuzingatia lishe bora.
“Tatizo la Shikizo la damu husababisha madhara makubwa ikiwemo kuharibu figo na macho, moyo kutanuka, na matatizo ya mishipa ya damu hivyo ni muhimu jamii ikafanya uchunguzi wa afya mara kwa mara na kuchukua tahadhari za mapema”, alisema Dkt. Manumbu.
Dkt. Manumbu alisisitiza umuhimu wa wananchi kujitokeza kwa wingi kila wanapopata fursa za huduma za uchunguzi wa magonjwa ya moyo bila malipo hususani huduma zinapofika katika maneno wanayoishi.
Dkt. Manumbu alisema watu 201 wamepewa rufaa ya kufika katika Taasisi hiyo kwaajili ya kufanyiwa uchunguzi zaidi na wengine kuanzishiwa matibabu ikiwemo kufanyiwa upasuaji wa moyo.
“Tusifuate mitandao ya kijamii katika kulinda afya zetu kwani sio watu wote wanaotoa ushauri wanamaarifa juu ya yale wanayoyasema, ni vema tukatumia fursa kama hii ya maonesho kupima afya zetu, kupata ushauri kutoka kwa wataalamu na kuzingatia maelekezo yanayotolewa na wataalamu”, alisema Dkt. Manumbu.
Dkt. Manumbu aliongeza kuwa baadhi ya wananchi waliobainika kuwa na magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo kisukari, shinikizo la juu la damu, matatizo ya mfumo wa umeme wa moyo na matatizo ya kuziba kwa mishipa ya damu walikuwa hawajui kama wanamatizo hayo jambo ambalo lingeweza kuleta madhara makubwa katika maisha yao.
Mwananchi aliyetembelea banda la JKCI kwaajili ya kufanyiwa uchunguzi wa afya Grace Ezekiel alisema maonesho ya madini yamemrahisishia kupata huduma za kibingwa za uchunguzi wa magonjwa ya moyo bila kutumia gharama, muda na kusafiri umbali mrefu kuzifua mahali zilipo.
“Nimefurahi kufanyiwa uchunguzi wa moyo na wataalamu wa JKCI kwani hapo awali niliwahi kufanyiwa uchunguzi wa moyo na hospitali za huku Geita na kutokuridhika na majibu lakini leo nimefika hapa na nimepewa majibu yaleyale, baada ya kufanya vipimo naanza kufuata ushauri niliopewa na wataalamu”, alisema Grace.
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imekuwa ikishiriki katika maonesho ya kitaifa ya teknolojia ya madini kwa lengo la kusogeza huduma bingwa bobezi karibu na wananchi na kuwasaidia watu wenye magonjwa hayo kupata matibabu kwa urahisi.
