Viongozi na wawakilishi wa mabunge kutoka mataifa mbalimbali duniani wameendelea kuwasili jijini Arusha kwa ajili ya kushiriki Mkutano wa 153 wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), utakaonza tarehe 5 Oktoba, 2026 jijini Arusha.

Viongozi hao wamewasili leo Oktoba 3, 2026 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) na Uwanja wa Ndege wa Arusha.

Miongoni mwa viongozi waliowasili ni Makamu wa Rais Mstaafu wa Malawi, Mheshimiwa Khumbo Kachali, Spika wa Bunge la Oman, Mheshimiwa Sheikh Khalid bin Hilal Al Maawali, na Naibu Spika wa Bunge la Palestina, Mheshimiwa Mussa Haddid.

Wengine waliowasili ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje katika Bunge la Bangladesh, Mheshimiwa Jahrat Adib Chowdhury, pamoja na ujumbe wake, na Mheshimiwa Sahiba Gafarova kutoka Bunge la Azerbaijan.

Mkutano wa IPU unawakutanisha washiriki zaidi ya 2,000 kutoka nchi mbalimbali duniani wanachama wa Umoja huo na utafanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano (AICC) jijini Arusha.

Ushiriki wa viongozi hao kutoka mabunge mbalimbali unaendelea kuifanya Arusha kuwa kitovu cha mikutano ya kimataifa, huku mkutano huo ukitoa fursa kwa wabunge kujadili masuala yanayogusa maendeleo, amani, ushirikiano na ustawi wa jamii duniani.