Mashindano ya mbio za magari ya Serengeti Rally of Tanzania 2026 yamezinduliwa rasmi mkoani Morogoro, huku magari yakitarajiwa kuanza kutimua vumbi kesho katika maeneo ya Msitu wa Shamba la Miti Morogoro.
Uzinduzi wa mashindano hayo umefanyika katika Kiwanda cha Serengeti, ukiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Mjini, Mhe. Mussa Kilakala, ambaye amewataka washiriki pamoja na watazamaji kuzingatia usalama wakati wote wa mashindano.
Mhe. Kilakala pia amesisitiza umuhimu wa kutunza mazingira, akiwataka washiriki, mashabiki na wananchi wanaokwenda kushuhudia mashindano hayo kuhakikisha shughuli zao haziathiri uoto wa asili na mazingira ya Msitu wa Shamba la Miti Morogoro.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Kamishna Msaidizi kutoka Kurugenzi ya Uzalishaji Mbegu za Miti, Dkt. Hamza Kateti, amesema Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) utaendelea kusimamia na kulinda mazingira ambayo ni sehemu muhimu ya kuwezesha shughuli mbalimbali kufanyika katika maeneo ya misitu.
Dkt. Kateti amewahimiza wananchi kutumia fursa hiyo pia kujifunza na kufanya utalii wa ikolojia, kwa kutembelea hifadhi na maeneo mbalimbali ya asili yanayopatikana mkoani Morogoro na yanayosimamiwa na TFS.
Kwa upande wa madereva watakaoshiriki mashindano hayo, wameeleza kuridhishwa na hali ya njia iliyotumika katika maandalizi ya mbio hizo, wakisema imekuwa na changamoto zinazohitajika kwa mashindano ya magari na hivyo kutoa ushindani wa kuvutia
Baadhi ya madereva wamesema wameiona njia hiyo na wamejiridhisha kuwa inawapa nafasi ya kuonyesha uwezo wao wa kuendesha magari katika mazingira yenye changamoto. Wamesema kila mmoja anaingia kwenye mashindano akiwa na lengo la kufanya vizuri na kuibuka mshindi.
Madereva hao wameeleza kuwa ushindani unatarajiwa kuwa mkubwa kutokana na ubora na changamoto za njia, huku kila mmoja akiamini kuwa mkakati wake, uzoefu na uwezo wa gari vitamwezesha kumaliza mbio hizo katika nafasi ya juu.

