WAKALA wa Nishati Vijijini (REA) umeendesha mafunzo kwa watendaji wa Serikali za Mitaa katika Halmashauri ya Nachingwea mkoani Lindi, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuongeza matumizi yenye tija ya umeme na kuhamasisha wananchi kutumia nishati safi ya kupikia.

Mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo watendaji wa Serikali za Mitaa ili waweze kutoa elimu kwa wananchi kuhusu namna ya kutumia umeme kwa ufanisi katika shughuli za uzalishaji na kiuchumi, pamoja na umuhimu wa kutumia nishati safi ya kupikia.

Akizungumza Afisa Maendeleo ya Jamii Mwandamizi wa REA, Bi. Jaina Msuya, amesema mafunzo hayo yanayotolewa katika wilaya mbalimbali za Mkoa wa Lindi yanalenga kuwapa watendaji ujuzi wa kuwaelimisha wananchi kuhusu fursa zinazopatikana kupitia matumizi ya umeme na nishati safi ya kupikia.

Amesema watendaji wa Serikali za Mitaa wana nafasi muhimu katika kufikisha elimu hiyo kwa wananchi, hususan katika kuwahamasisha kutumia nishati ya umeme kuongeza uzalishaji, kipato na kuboresha maisha.

Kwa upande wao, wawakilishi wa taasisi za fedha, Benki ya NMB kupitia Afisa Mikopo wake, Bw. Jacob Mwashusa na NBC kupitia Meneja wake wa Mkoa wa Lindi, Bw. Loving Mapunda, wameeleza fursa za kifedha zinazopatikana kwa wananchi na wajasiriamali, ikiwemo mikopo yenye masharti nafuu kwa ajili ya kuanzisha na kukuza shughuli za kiuchumi zinazotumia umeme.

Aidha, Mtaalam Mwelekezi kutoka Kampuni ya Dar es Salaam Merchant Group, Bi, Hermina Chonya ambayo ni mtoa huduma wa mafunzo hayo katika Mkoa wa Lindi ametoa elimu kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia na kueleza namna majiko yenye ufanisi yanavyoweza kusaidia kupunguza matumizi ya kuni na mkaa.

Amesisitiza kuwa matumizi ya nishati safi ya kupikia yanachangia kupunguza athari za mazingira na kuongeza ufanisi katika matumizi ya nishati majumbani na kwenye shughuli mbalimbali za uzalishaji.

Mafunzo hayo ni sehemu ya mpango wa REA wa kuwajengea uwezo viongozi na watendaji wa Serikali za Mitaa ili waweze kuwa kiungo muhimu katika kuhamasisha jamii kutumia umeme kwa tija na kuachana na matumizi ya nishati zisizo safi za kupikia.