Waziri wa Ujenzi, Masanja Kadogosa, ameutaka Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), wakandarasi na washauri elekezi wanaosimamia ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa muda uliopangwa.

Kadogosa alitoa agizo hilo alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa uwanja huo, ambapo amesema uwanja huo ni miongoni mwa miradi mikubwa inayotekelezwa nchini na una umuhimu mkubwa katika kuifanya Dodoma kuwa Makao Makuu yenye miundombinu ya kisasa.

“Unajua watu wanapoambiwa Uwanja wa Msalato wanaona kama ni kitu kidogo, lakini ni mkubwa sana. Ukishakuja hapa ndipo unaweza kuuthamini ukubwa wa uwanja huu,” alisema.

Kadogosa alisema licha ya changamoto zilizopo, maendeleo ya mradi yanaridhisha na Serikali itaendelea kufuatilia utekelezaji wake ili kuhakikisha muda uliokubaliwa unazingatiwa.

“Tunapokubaliana jambo, kama tumesema Novemba iwe Novemba. Kama tumesema Desemba iwe Desemba,” alisema.

Aliwataka wakandarasi kutoa taarifa sahihi kuhusu muda wa kukamilisha kazi, akisisitiza kuwa taarifa hizo hutumika kutoa mrejesho kwa viongozi wakuu wa Serikali.

Aidha, aliiagiza TANROADS na washauri elekezi kusimamia kwa karibu ujenzi wa jengo la abiria, barabara ya kurukia na kutua ndege pamoja na miundombinu mingine muhimu.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Ujenzi, Godfrey Kasekenya, alisema uwanja huo ni miongoni mwa viwanja vya kisasa nchini na umejengwa kwa namna inayowezesha kuongeza uwezo wake kulingana na mahitaji.

Kwa mujibu wa msimamizi wa mradi, Meshack Kabote, ujenzi wa miundombinu umefikia asilimia 88, huku majengo ukiwa asilimia 79.5. Alisema miundombinu inatarajiwa kukamilika mwishoni mwa Novemba, huku majengo yakitarajiwa kukamilika mwishoni mwa Desemba.