Geita 02 Oktoba 2026
Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Madini Tanzania (FEMATA), Bw. John Wambura Bina, amepongeza juhudi za Tume ya Ushindani (FCC) katika kusimamia utekelezaji wa sheria ya ushindani na kuhakikisha misingi ya ushindani wa haki inazingatiwa katika sekta ya madini.
Bw. Bina ameyasema hayo baada ya kutembelea banda la Kliniki ya Biashara, linaloshirikisha taasisi mbalimbali za Serikali, ikiwemo FCC, wakati wa Maonesho ya Tisa ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea mkoani Geita.
Akiwa katika banda hilo, Bw. Bina alipata maelezo kutoka kwa Bw. Nsajigwa Wilfred, Afisa Uhusiano wa Umma Mkuu wa FCC, kuhusu majukumu ya Tume, utekelezaji wa sheria ya ushindani pamoja na mchango wa FCC katika sekta ya madini.ñ
Aidha, alitembelea sehemu mbalimbali za banda hilo na kujionea bidhaa zinazozalishwa na wafanyabiashara na wazalishaji wa Kitanzania, pamoja na kupata taarifa kuhusu huduma zinazotolewa na taasisi mbalimbali kwa Umma.
Bw. Bina amesema ushiriki wa FCC katika maonesho hayo ni muhimu kwakuwa unatoa fursa ya kuwafikia moja kwa moja wachimbaji, wafanyabiashara na wadau wengine wa sekta ya madini, kuwapatia elimu kuhusu masuala ya ushindani na kuwawezesha kuendesha biashara zao kwa kuzingatia misingi ya ushindani wa haki.
Amesema hatua hiyo ni muhimu katika kuimarisha biashara na kuchangia ukuaji wa uchumi wa soko nchini.
Akieleza kuhusu majukumu ya FCC na mchango wa Tume katika sekta ya madini katika kipindi cha hivi karibuni, Bw. Nsajigwa amesema FCC iliridhia miamala ya ununuzi wa baadhi ya hisa katika kampuni zinazohusika na miradi ya madini, hatua inayolenga kuwezesha uwekezaji na kuchochea uzalishaji wa madini nchini.
Ameeleza kuwa miongoni mwa miamala hiyo ni kampuni ya Shudao Investment Group Co., Ltd kununua baadhi ya hisa za Tanzania China International Mineral Resources Limited (TCIMRL), kampuni inayotekeleza Mradi wa Makaa ya Mawe wa Mchuchuma pamoja na Mradi wa Madini ya Chuma wa Liganga, unaohusisha uzalishaji wa chuma (steel), wenye thamani inayozidi Dola za Marekani bilioni 2.3.
Kwa mujibu wa Bw. Nsajigwa, Shudao Investment Group Co., Ltd inamilikiwa na Tume ya Usimamizi na Utawala wa Mali ya Serikali ya Mkoa wa Sichuan, China.
Ameeleza kuwa kutokana na uzoefu wa kampuni hiyo katika usimamizi wa miradi ya madini ya chuma, uwezo wake wa kiteknolojia pamoja na nguvu zake za kifedha, ushirikiano huo unaweka msingi wa maendeleo na uendeshaji endelevu wa miradi ya Liganga na Mchuchuma.
Bw. Nsajigwa pia ameeleza kuwa FCC iliridhia ununuzi wa baadhi ya hisa za Mamba Minerals Corporation Limited na kampuni ya Shenghe Resources Co., Limited.
Amesema Mamba Minerals Corporation Limited ni kampuni ya ubia kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Ngualla Group UK Limited, inayosimamia Mradi wa Madini ya Ardhi Adimu (Rare Earth Minerals) wa Ngualla.
Kwa mujibu wa maelezo hayo, muungano huo unalenga kukuza uwezo wa kibiashara na ushindani wa kimataifa wa Mradi wa Ngualla, ambao unakadiriwa kuwa na uwekezaji wa mtaji wa takriban Dola za Marekani milioni 320.
Aidha, mradi huo unatarajiwa kutoa manufaa ya kijamii na kiuchumi, ikiwemo kuunda takriban ajira 600 za moja kwa moja na 3,000 zisizo za moja kwa moja wakati wa ujenzi, pamoja na takriban ajira 220 za moja kwa moja na 1,000 zisizo za moja kwa moja wakati wa uendeshaji.
Bw. Nsajigwa amesema FCC imeendelea kuhakikisha kuwa ununuzi wa kampuni ndogo za madini, hususan zile zinazomilikiwa na wazawa, unafanyika kwa kuzingatia matakwa ya sheria ya ushindani.
Amesema hatua hiyo inalenga kuhakikisha kuwa miamala ya kibiashara katika sekta ya madini inazingatia sheria na kwamba ushindani wa haki unaendelea kuwepo katika soko.
Baada ya kupokea maelezo kuhusu mchango wa FCC katika sekta ya madini, Rais wa FEMATA, Bw. Bina, ameonesha haja ya kufungua ukurasa mpya wa ushirikiano wa kiutendaji kati ya FCC na FEMATA.
Amesema ushirikiano huo utasaidia taasisi hizo kushughulikia kwa pamoja masuala mbalimbali yanayowakabili wachimbaji madini, ikiwemo changamoto za kibiashara na uhitaji wa elimu kuhusu masuala ya ushindani.
Kwa mujibu wa Bw. Bina, kuwepo kwa utaratibu mzuri wa kuwafikishia wachimbaji madini elimu ya ushindani kutawawezesha kuimarisha biashara zao, kuongeza uelewa wa sheria na kuchangia katika maendeleo ya uchumi jumuishi.
Katika hatua hiyo, Bw. Bina amemuelekeza Bw. Haroun Athuman Kinega, Mtendaji Mkuu wa FEMATA na Kamishna wa Tume ya Madini, kuwasiliana na FCC na kuweka utaratibu utakaowezesha taasisi hizo mbili kushirikiana kwa karibu kiutendaji.
Amesema ushirikiano huo unapaswa kulenga maslahi mapana ya wachimbaji madini, maendeleo ya biashara na ustawi wa uchumi wa soko nchini Tanzania.
Maonesho ya Tisa ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini yanaendelea mkoani Geita, yakitoa fursa kwa wadau wa sekta ya madini, wafanyabiashara, wazalishaji na wananchi kujifunza kuhusu teknolojia na huduma mbalimbali, kutangaza bidhaa na huduma zao, pamoja na kujenga mitandao ya kibiashara.
FCC inaendelea kushiriki katika maonesho hayo kupitia Kliniki ya Biashara, ambapo wafanyabiashara na wazalishaji wa bidhaa za Kitanzania wanapatiwa elimu na huduma kuhusu masuala ya ushindani, hususan udhibiti wa bidhaa bandia, ushindani wa haki na ulinzi wa mlaji.
Ushiriki wa FCC katika maonesho hayo unaendelea kutoa fursa kwa wadau wa sekta ya madini na wafanyabiashara kupata uelewa kuhusu haki na wajibu wao chini ya sheria ya ushindani, sambamba na kuimarisha mazingira ya biashara na uchumi wa soko nchini.
