

Mkurugenzi wa Enabel nchini Tanzania Bi. Virginie Hallet akisini hati za makubaliano ya ushirikiano (MoU) na Tanzania Innovation Hubs Network (THN) pamoja na Zanzibar Startup Association (ZSA), kwa lengo la kuimarisha mifumo ya ubunifu, ujasiriamali wa kidijitali iliyofanyika jijini Dar es Salaam

Meneja wa Mradi wa Africa-Europe Digital Innovation Bridge wa Enabel, Joachim Mangilima akizungumza na waandishi wa habari kuhusu umuhimu wa mradi huo

Mkurugenzi wa Enabel nchini Tanzania Bi. Virginie Hallet, Mtendaji Mkuu wa Zanzibar Startup Association (ZSA), Ikram R. Soragha, Mkurugenzi Mtendaji wa Tanzania Innovation Hubs Network (THN), Kiko Kiwanga, wakiwa katika picha ya pamoja wakiwa wameshika hati za makubaliano ya ushirikiano (MoU)
…………
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Wakala wa Maendeleo wa Ubelgiji (Enabel) umesaini hati mbili za makubaliano ya ushirikiano (MoU) na Tanzania Innovation Hubs Network (THN) pamoja na Zanzibar Startup Association (ZSA), kwa lengo la kuimarisha mifumo ya ubunifu, ujasiriamali wa kidijitali na ushirikiano kati ya Afrika na Ulaya.
Makubaliano hayo pia yanalenga kurahisisha utekelezaji wa malengo ya Enabel kupitia programu zinazozingatia maarifa ya ndani na vipaumbele vya wabunifu na wajasiriamali.
Akizungumza katika hafla ya utiaji saini iliyofanyika jijini Dar es Salaam, Meneja wa Mradi wa Africa-Europe Digital Innovation Bridge wa Enabel, Joachim Mangilima, amesema ushirikiano huo utasaidia kuboresha mazingira ya ubunifu na kuongeza uwezo wa wajasiriamali wa kidijitali.
Amesema mradi huo utaunganisha wajasiriamali na wawekezaji kutoka Ulaya, huku ukilenga kukuza biashara endelevu, kuongeza ajira na kuwezesha ubunifu wa suluhisho zinazolenga kukabiliana na changamoto mbalimbali za jamii.
“Kwa sasa tumechagua Nchi ya Tanzania, Uganda na Senegal katika utekelezaji wa mradi huu. Mashirika ambayo tumeingia nayo makubaliano yatatusaidia kurahisisha utekelezaji wa malengo yetu,” amesema Mangilima.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Zanzibar Startup Association (ZSA), Ikram R. Soragha, amesema ushirikiano huo utasaidia kujenga mazingira wezeshi kwa vijana kutumia ubunifu wao katika kuanzisha na kukuza biashara.
Amesema ZSA itashiriki katika kusimamia utekelezaji wa mradi huo, ambao utakuwa kiungo muhimu katika kukuza mahusiano ya kibiashara na ubunifu kati ya Afrika na Ulaya.
“Mradi huu utaangalia mambo mbalimbali, ikiwemo sera na sheria,” amesema Soragha.
ZSA inawakilisha kampuni changa na wabunifu wa kidijitali kutoka Zanzibar, Unguja na Pemba, na itakuwa mshirika muhimu wa Enabel katika kushirikisha jamii katika utekelezaji wa programu hiyo.
Ushirikiano huo utaanza kwa kutambua wadau na kuchambua hali ya mazingira ya ubunifu nchini, pamoja na kukusanya taarifa za msingi. Pia utahusisha uhamasishaji wa wadau, kubadilishana maarifa na kukuza ujasiriamali, hususan ushiriki wa wanawake na vijana.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Tanzania Innovation Hubs Network (THN), Kiko Kiwanga, amesema ushirikiano huo utasaidia kuboresha shughuli zinazotekelezwa na mtandao huo, ikiwemo kujenga uwezo wa vituo vya ubunifu nchini.
THN inaunganisha na kuimarisha vituo vya ubunifu wa kidijitali na kiteknolojia nchini Tanzania, huku ushirikiano huo ukilenga kutumia mtandao na maarifa yake kuboresha programu za Enabel na kuimarisha uwezo wa vituo wanachama.
Aidha, shughuli hizo zitahusisha kukuza ubunifu wa kidijitali, ujasiriamali jumuishi na uchumi wa kijani, pamoja na kubadilishana tafiti na taarifa kuhusu sera, kushiriki mikutano ya wadau na kuandaa machapisho ya maarifa kwa pamoja.
Ushirikiano huo unatarajiwa pia kuchangia utekelezaji wa azma ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ya kujenga uchumi imara, jumuishi na shindani unaochochewa na ubunifu, mageuzi ya kidijitali na ujuzi.
