Na Mwamvua Mwinyi, Kibaha
MKUU wa Mkoa wa Pwani, Stanslaus Haroon Nyongo, amewaagiza Wakuu wa Wilaya zote mkoani humo kuhakikisha migogoro ya ardhi inayowakabili wananchi inatatuliwa kwa wakati na kwa kuzingatia sheria.
Nyongo ametoa maagizo hayo leo, Oktoba 3, 2026, katika hafla iliyofanyika Kibaha wakati wa kumuapisha Mkuu wa Wilaya ya Kibiti, Luteni Kanali Fortunatus Beda Kipeta, akieleza kuwa migogoro ya ardhi imeendelea kuwa miongoni mwa changamoto kubwa zinazokabili Mkoa wa Pwani.
Amesema baadhi ya watu wamekuwa wakinufaika na uwepo wa migogoro hiyo, huku baadhi ya watumishi wasio waaminifu wakichangia kuibuka na kuendelea kwa migogoro hiyo, hali inayohitaji viongozi kuchukua hatua stahiki ili kuhakikisha wananchi wanapata haki zao kwa mujibu wa sheria.
“Mkoa wa Pwani ni mkoa wa kimkakati na unaendelea kuvutia wawekezaji wengi, Hatuwezi kuwa na mazingira mazuri ya uwekezaji kama hatutatatua migogoro ya ardhi, azima viongozi wetu tushughulikie changamoto hizi kwa umakini na kwa wakati,” amesema Nyongo.
Aidha Nyongo amezitaka Halmashauri zote za Mkoa wa Pwani kuanzisha vituo maalum vya mauzo ya ardhi vitakavyowaunganisha wamiliki halali wa ardhi na wawekezaji, ili kurahisisha upatikanaji wa ardhi kwa njia rasmi, salama na inayozingatia sheria.
Amesema utaratibu huo unalenga kuweka mazingira bora ya uwekezaji na kurahisisha upatikanaji wa maeneo kwa wawekezaji, sambamba na kuhakikisha shughuli za mauzo ya ardhi zinafanyika kwa kufuata taratibu na sheria zilizowekwa.
Kadhalika amezitaka Halmashauri kuongeza juhudi katika ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa kubuni vyanzo vipya vya mapato na kutumia kikamilifu fursa zilizopo katika maeneo yao.
Amesisitiza kuwa mapato ya ndani ni muhimu katika kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi na kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo, hivyo Halmashauri zinapaswa kutumia fursa zilizopo kuongeza uwezo wa kifedha.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kibiti, Luteni Kanali Fortunatus Beda Kipeta, ameahidi kutekeleza kwa vitendo maelekezo yote yaliyotolewa na Mkuu wa Mkoa, huku akisisitiza kuwa atasimamia watendaji wa Wilaya hiyo kufanya kazi kwa nidhamu, weledi na kuzingatia maslahi ya wananchi.
Kipeta amesema atahakikisha kunakuwa na utaratibu mzuri wa kuwasikiliza wananchi, kupokea changamoto zao na kuzitafutia ufumbuzi kwa wakati, sambamba na kuhakikisha wananchi wanashirikishwa na kunufaika na fursa mbalimbali za maendeleo zilizopo katika Wilaya ya Kibiti.

