NA DENIS MLOWE, IRINGA
MBUNGE wa Jimbo la Kalenga, Jackson Kiswaga, amekutana na kula chakula cha pamoja na wanafunzi wenye mahitaji maalum katika Shule ya Msingi Kipera, iliyopo Kata ya Nzihi, Jimbo la Kalenga, akisema hatua hiyo inalenga kuwapa faraja na kuwafanya wajione kuwa sehemu muhimu ya jamii
Kiswaga alitoa kauli hiyo baada ya kushiriki chakula cha pamoja na wanafunzi hao, ambapo alisema Serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imefanya uwekezaji katika kituo hicho kwa lengo la kuhakikisha watoto wenye mahitaji maalum wanapata elimu na malezi bila kutengwa.
Alisema shule hiyo imekuwa ikipokea watoto wenye mahitaji maalum kutoka maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Iringa, wakiwamo wanaotoka wilayani Mufindi, Kilolo, Iringa Vijijini na maeneo mengine.
“Tunashukuru Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa na kituo kama hiki ambacho serikali imewekeza kwa ajili ya kuwalea watoto wenye mahitaji maalum hapa kuna watoto kutoka Mkoa mzima wa Iringa wenye changamoto mbalimbali, wakiwamo wenye uoni hafifu na changamoto nyingine,” alisema Kiswaga.
Kiswaga alisema ameamua kutumia muda wake kukaa na watoto hao na kula nao chakula kwa pamoja kutokana na kuamini kuwa wanahitaji upendo, faraja na kuhisi kuwa wanakubalika katika jamii.
Alisema watoto hao hawapaswi kujiona kuwa wametengwa na jamii kwa sababu Serikali inawatambua na inaendelea kuweka mazingira ya kuwawezesha kupata elimu na kufikia malengo yao ya maisha.
Kiswaga pia aliwataka viongozi, wafanyabiashara na wadau wengine kujitokeza kusaidia shule hiyo, akisema bado kuna mahitaji mbalimbali yanayohitaji nguvu ya pamoja ili kuboresha mazingira ya kujifunzia na kuishi kwa wanafunzi.
“Nitaendelea kufanya hivi kila mwaka, hasa katika siku maalum za kula nao chakula, lakini pia tunawakaribisha wenzangu wengine walio katika maeneo mbalimbali kuja hapa Shule ya Msingi Kipera, kuwaona watoto hawa na kuchangia mahitaji mbalimbali,” alisema.
Kwa upande wake, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kipera, Faines Mteleka, alisema shule hiyo ilianzishwa mwaka 1976 na kwa sasa ina wanafunzi 609, wakiwamo wanafunzi 145 wenye mahitaji maalum.
Alisema kituo cha watoto wenye mahitaji maalum katika shule hiyo kilianzishwa kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Mkoa wa Iringa na Serikali ya Wilaya, kwa lengo la kuwapa huduma watoto wenye mahitaji mbalimbali bila kuwalazimisha kusafiri umbali mrefu kutafuta elimu.
Mteleka alisema wanafunzi hao wana changamoto mbalimbali, zikiwamo za uoni, usikivu, ulemavu wa akili, usonji, ualbino na ulemavu wa viungo.
Alisema wanafunzi wenye mahitaji maalum wanaopokelewa shuleni hapo wanatoka ndani na nje ya Mkoa wa Iringa, huku Serikali ikigharamia mahitaji yao muhimu wanapokuwa shuleni hapo.
Mteleka, alisema kuwa wanafunzi hao hawalipi ada wala michango ya shule, huku Serikali ikigharamia chakula cha asubuhi, mchana na jioni pamoja na mahitaji mengine ya malezi.
Alisema pia Serikali imeweka walezi, wakiwamo walezi wa kiume na wa kike, wanaowahudumia wanafunzi hao mchana na usiku, sambamba na walimu wanaowapa elimu kulingana na mahitaji na changamoto walizonazo.
Pamoja na mafanikio hayo, Mwalimu Mkuu alisema shule hiyo bado inakabiliwa na changamoto kadhaa, ikiwamo upungufu wa walimu wenye uwezo wa kuhudumia idadi kubwa ya wanafunzi wenye mahitaji tofauti.
Mteleka alisema shule hiyo pia inaendelea kukabiliwa na changamoto ya miundombinu, hasa ukumbi wa chakula ambao bado haujakamilika hivyo kukamilika kwa ukumbi huo kutasaidia kuboresha huduma za chakula kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum pamoja na wanafunzi wengine wa shule hiyo.
Alisema licha ya Serikali kufanya juhudi kubwa katika kuboresha huduma shuleni hapo, bado mchango wa wadau mbalimbali unahitajika katika kukamilisha miundombinu na mahitaji mengine.
Mteleka alimshukuru Mbunge Kiswaga kwa kutenga muda wa kutembelea shule hiyo na kukutana na wanafunzi, akisema ziara hiyo siyo ya kwanza kwake kwani amewahi kufika shuleni hapo na kushiriki katika shughuli mbalimbali za kuwasaidia wanafunzi.
Alisema ushirikiano kutoka kwa viongozi wa ngazi mbalimbali, Serikali na wadau wengine umeendelea kuboresha maisha ya wanafunzi na walimu katika shule hiyo.

