Na. S’sgt Mawazo Mtondo – MWANZA
Timu ya mpira wa wavu wanawake ya Jeshi la Magereza imehitimisha kwa kishindo ushiriki wake katika Mashindano ya Baraza la Michezo ya Majeshi Tanzania (BAMMATA) 2026, baada ya kuibuka na ushindi wa seti 3–0 dhidi ya timu ngumu ya Ngome ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).
Mchezo huo, uliokuwa wa ushindani mkubwa ukihusisha mbinu, mipango na umakini wa hali ya juu kutoka kwa pande zote mbili, umefanyika leo Oktoba 1, 2026 katika Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.
Ushindi huo umeiwezesha timu ya wanawake ya Kanda ya Magereza kutwaa ubingwa wa mpira wa wavu wanawake BAMMATA 2026, baada ya kuonyesha kiwango bora katika michezo yake yote.
Katika michezo yake ya awali timu hiyo, iliifunga Polisi wanawake kwa seti 3–0, kabla ya kuendeleza kasi hiyo kwa kuichapa timu ya SMZ kwa seti 3–0. Katika mchezo mwingine, Magereza iliibuka na ushindi wa seti 3–1 dhidi ya JKT Tanzania.
Matokeo hayo yameifanya timu ya wanawake ya Kanda ya Magereza kumaliza mashindano ikiwa mabingwa wa mpira wa wavu wanawake kwa kutopoteza mchezo hata mmoja katika mashindano ya BAMMATA 2026, huku ikionesha uwezo mkubwa katika mashindano hayo.
