▪️Wahimizwa kujiandaa kutumia Mfumo wa Kidijiti wa e-Ardhi.

Wananchi zaidi ya 60 ambao wamekamilisha taaratibu za kumilikishwa ardhi ya viwanja vyao kupitia zoezi la urasimishaji makazi katika eneo la Klyamatundu halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga wameandaliwa na kukabidhiwa hatimiliki zao kupitia Kliniki ya Ardhi inayoandelea katika eneo hilo.

Zoezi hilo la kukabidhiwa hatimiliki, limefanywa tarehe 29 Septemba, 2026 na Ofisi ya Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Rukwa likiongozwa na Mkurugenzi Msaidizi wa Urasimishaji Makazi Bw. Nicholaus Mwakasege kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi katika Viwanja vya Ofisi za Serikali ya Mtaa, Klyamatundu.

Akiwapongeza wananchi waliopata hati zao kupitia kliniki inayoendelea, Bw. Mwakasege ametoa wito kwa wananchi wote kujiandaa na mabadiliko ya kutumia Mfumo wa Kidijiti wa e-Ardhi kwa kuwa Serikali imedhamiria na iko katika hatua nzuri ya kufanya mageuzi makubwa ya matumizi ya TEHEMA katika utoaji wa huduma za sekta ya ardhi nchini kupitia mfumo uliojengwa na watalaam wa ndani wa e-Ardhi.  

Aliongeza kwa kueleza kuwa utoaji wa huduma za ardhi kupitia mfumo wa e-ardhi kutarahisisha upatikanaji wa huduma za ardhi na kuokoa kwa kupunguza muda wa wananchi ambao wamekuwa wakiutumia katika kufuatilia huduma za ardhi kwa kuwa mfumo utatoa fursa ya kupata huduma za ardhi ukiwa popote pale kwa kuwasilisha maombi yako kidijiti.