Mwalimu Mkuu wa shule hiyo ya Arusha Intergrated ,Rems Munyuku akizungumza kwenye mahafali hayo jijini Arusha


Askofu wa kanisa la Arusha Revival Christian Center ,Askofu Mch ,David Mollel akimkabidhi cheti mmoja wa wahitimu katika mahafali hayo jijini Arusha
………….
Na Happy Lazaro, Arusha
WAHITIMU nchini wametakiwa kumtanguliza Mungu katika maisha yao, kuwa na ndoto kubwa, kuweka bidii katika masomo na kujenga nidhamu ili waweze kufikia malengo yao na kufanikiwa katika safari yao ya elimu na maisha.
Hayo yemesemwa jijini Arusha na Askofu wa kanisa la Arusha Revival Christian Center ,Askofu Mch ,David Mollel katika mahafali ya 15 katika shule ya mchepuo wa kiingereza ya Arusha Intergrated ambapo jumla ya wanafunzi 21 wamehitimu darasa la saba .
Askofu Mollel amewashukuru wazazi kwa mchango wao katika kuwawezesha watoto wao kufikia hatua hiyo, ikiwemo kulipa ada, kugharamia mahitaji mbalimbali na kusimama nao kwa kipindi cha miaka saba na zaidi tangu walipoanza elimu yao.
Aidha amewataka kutoridhika na kuishia katika elimu ya msingi bali waendelee kusoma hadi kufikia viwango vya juu ndani na nje ya Tanzania.
Amewahimiza wahitimu kumtanguliza Mungu katika maisha yao kwa kushiriki ibada na kuishi maisha yanayompendeza, akisema msingi huo utawasaidia katika safari yao ya maisha.
Aidha Askofu Mollel amewasihi kuwa na ndoto kubwa, wakijiwekea malengo ya kuwa madaktari, wanasheria, walimu, wahandisi, marubani na viongozi wa baadaye.
Aidha amewataka wahitimu kuweka bidii katika masomo, akisisitiza kuwa mafanikio hayawezi kupatikana bila juhudi na kuwataka kusoma kwa bidii na kutokata tamaa wanapokutana na changamoto, bali kuwa na ujasiri wa kuendelea kupambana hadi kufikia malengo yao.
Askofu Mollel amesema kuwa wahitimu wanapaswa kutambua kuwa nidhamu ndio nguzo muhimu ya mafanikio, na kusema kuwa safari ya elimu na maisha kwa ujumla inahitaji mtu kujua mambo ya kushikamana nayo na yale anayopaswa kuyaacha.
Amewataka wahitimu kuepuka mienendo isiyofaa na kujenga tabia zitakazowasaidia kuwa watu wenye heshima na mchango katika jamii.
Askofu Mollel ameahidi kanisa hilo kuendelea kuboresha shule, hususani katika eneo la elimu na miundombinu, baada ya baadhi ya changamoto kutajwa katika risala ya wahitimu.
“Kanisa limejipanga kuhakikisha mazingira ya shule yanaendelea kuwa bora kwa wanafunzi ambapo hatua za maboresho tayari zimeanza, mfano mzuri ni jiko la shule ambalo awali lilikuwa chakavu lakini limefanyiwa maboresho.”amesema Askofu Mollel .
Askofu Mollel amesema kuwa, jitihada hizo zinalenga kuboresha mazingira ya kujifunzia na kuhakikisha wanafunzi wanapata huduma bora zaidi wakati wakiendelea na safari yao ya elimu.
Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa shule hiyo ya Arusha Intergrated ,Rems Munyuku ametoa wito kwa wazazi na walezi kuchagua shule zinazosisitiza elimu, nidhamu na maadili mema kwa watoto ambapo amesema shule hiyo inatoa elimu kuanzia madarasa ya awali kwa watoto wenye umri wa miaka miwili hadi darasa la Saba.
Munyuku amesema kuwa , shule hiyo inayomilikiwa na kanisa la Arusha Revival Christian Center imejikita katika kutoa elimu pamoja na kujenga nidhamu na maadili bila kubagua wanafunzi kwa misingi ya dini.
Ameongeza kuwa ,wazazi na walezi wanapaswa kuzingatia zaidi shule zinazoweza kuwajenga watoto kitaaluma na kitabia,huku akisisitiza kuwa shule hiyo inaendelea kuweka mkazo katika malezi yenye maadili yanayoweza kuwa msingi wa maisha yao ya baadaye.
Aidha amefafanua kuwa, shule hiyo inatoa nafasi kwa wazazi wenye uwezo tofauti kutokana na ada yake kuwa nafuu na kuruhusu malipo kufanyika kwa awamu nne, huku ikiwa na huduma ya usafiri kwa wanafunzi wanaotoka maeneo ya pembezoni mwa jiji la Arusha.
Amewataka kuendelea na masomo na kujifunza zaidi baada ya kumaliza elimu ya msingi, kwani mabadiliko ya mitaala na masomo yanahitaji wanafunzi kuendelea kujiongezea maarifa ili kukabiliana na hatua zinazofuata za elimu.
Aidha amesisitiza kuwa wahitimu hao hawapaswi kuishia katika mafanikio ya kumaliza Darasa la Saba pekee, bali waendelee kujijenga katika taaluma, maadili na nidhamu ili kuwa vijana wenye mchango chanya katika jamii na kufanikiwa katika elimu ya sekondari na maisha yao ya baadaye.
